2015-04-21 07:13:00

Biashara haramu ya binadamu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!


Baba Mtakatifu Francisko anasikitishwa sana na ongezeko la biashara haramu ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia, jambo ambalo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Huu ni utamaduni wa kifo unaojichimbia katika mchakato a kutafuta utajiri wa haraka haraka, kielelezo cha utandawazi usiojali wa kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Haya  yamesemwa na Askofu mkuu Marcelo Sànchez Sorondo, mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii katika mkutano wa Taasisi hii uliofunguliwa hapo tarehe 17 na kuhitimishwa tarehe 21 Aprili 2015. Mkutano huu wa kawaida umeongozwa na tema “Biashara haramu ya binadamu: tatizo linalovuka uhalifu”.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna zaidi ya watu millioni mbili, wengi wao wakiwa ni wanawake na wasichana, wanaoendelea kutumbukizwa katika utumwa mamboleo, kwa kufanyishwa ukahaba na matajiri ili kukidhi soko la utalii wa ngono duniani. Itakumbukwa kwamba, Protokali ya Palermo, iliyopitishwa kunako mwaka 2003, ilipiga rufuku biashara haramu ya binadamu. Hadi leo hii kuna zaidi ya watu millioni ishirini ambao hawajulikani mahali walipo.

Hili ni tatizo kubwa la kimataifa linalopaswa kufanyiwa kazi kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa karibu zaidi. Umaskini, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka ni kati ya vyanzo vikuu vya biashara haramu ya binadamu duniani. Hii inatokana na sababu kwamba, haki, mafao ya wengi, utu  na heshima ya binadamu, havijapewa kipaumbele cha kutosha katika sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji ya binadamu kama sehemu ya mchakato wa mikakati ya kiuchumi katika uzalishaji na utoaji  wa huduma. Soko huria bila kanuni maadili, ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya watu wengi duniani. Bado kuna ukosefu wa haki msingi za kijami na wakati mwingine, misaada ya kiuchumi na kijami inaambatana na masharti ambayo wakati mwingine yanakwenda kinyume cha kanuni maadili na utu wema, kwa kisingizio cha kutaka kukuza na kuendeleza uhuru na demokrasia.

Askofu mkuu Sànchez Sorondo anasema Kanisa linaendelea kuwafunda watu ili waishi kwa kiasi, katika haki, kwa kuangalia mafao na ustawi wa wengi. Maliasili na utajiri wad unia, unapaswa kutumiwa vyema kwa ajili ya wengi na wala si kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache ndani ya jamii. Haki jamii inajikita katika kanuni ya dhahabu ambayo inawahamasisha watu kutenda kadiri wanavyotaka kutendewa pia. Kile ambacho wewe hutaki kutendewa, kamwe usimtende jirani yako anasema Askofu mkuu Sànchez Sorondo.

Watu wanapaswa kutambua na kukiri uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, changamoto ya kuheshimiana, kupendana na kusaidiana kama ndugu. Vijana wa kizazi kipya washirikiana na wazee ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kutetea utu na heshima ya binadamu, badala ya mwelekeo wa sasa unaojikita katika uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka, chanzo kikuu cha majanga kwa mwanadamu. Watu wajifunge kibwebwe kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai, kwa kutambua kwamba, leo na kesho iliyo bora zaidi iko mikononi mwa vijana, lakini hekima na busara inajikita katika maisha ya wazee.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.