2015-04-20 07:29:00

Utume kwa Vijana: Kanisa litaendelea kuwekeza katika majiundo makini


Mama Kanisa bado anaendelea kuonesha ile sura ya huruma kwa vijana kama alivyofanya Yesu mwenyewe na kwamba, Kanisa linapenda kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, ili kuwawezesha vijana kupata majiundo makini: kitamaduni na kitaaluma mintarafu mwanga wa Injili. Dhamana hii imeendelea kutekelezwa na Kanisa kwa njia ya watoto wake waliojipambanua kwa kuwekeza katika elimu Katoliki katika sekta ya elimu, ili kutoa fursa ya majiundo makini ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Lengo hili linaweza kufikiwa kwa njia ya mchakato wa kisayansi unaojikita katika ukweli na rasilimali akili inayoongozwa na mwanga wa imani. Huu ndio utume ambao unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, matunda ya kazi ya mikono ya Padre Agostino Gemelli, ambaye kwa miaka mingi anajipambanua kuwa ni rejea makini katika majiundo ya vijana wa kizazi kipya kwenye Vyuo vikuu. Ni kiongozi ambaye amekuwa karibu na maisha ya wananchi wengi wa Italia, ambao wamguswa na huduma makini inayotolewa na Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na tafakari za kina zinaoendeshwa mara kwa mara Chuoni hapo.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwenda kwa Kardinali Angelo Scola, Rais wa Taasisi ya Elimu ya Giuseppe Toniolo, inayosimamia na kuendesha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, wakati wa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 91 tangu Chuo hiki kilipoanzishwa. Maadhimisho haya yanafanyika tarehe 19 Aprili 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, kutoka pembezoni hadi kati kati”.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, vijana ni kati ya waathirika wakuu wa myumbo wa uchumi kimataifa, kwani hawana tena uhakika wa fursa za ajira na hivyo kuwafanya kuwa na mashaka katika majiundo ya taaluma wanazoendelea kuzifanyia kazi wakati huu wakiwa vyuoni na kwamba, wanaona pia vigumu kuanzisha misingi ya familia; mambo ambayo yana madhara makubwa kwa jamii nzima. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuamka na kujifunga kibwebwe ili waweze kuonesha tena “jeuri” katika maisha ya kijamii, bila kukata wala kukatishwa tamaa, bali kusonga mbele, tayari kukabiliana na changamoto za maisha.

Changamoto ni sehemu ya maisha zinazokabiliwa kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa watu kujihusisha kikamilifu, daima wakisimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Wajifunge kibwebwe kupambana na umaskini wa hali na kipato, kwa kuimarisha utashi unaongozwa na mwanga wa Injili. Kanisa lina dhamana ya kuhakikisha kwamba, linatoa vitendea kazi muhimu ili kupambana na changamoto za maisha: kimaadili na kitamaduni na kwamba, utandawazi uwawezeshe kuwa ni wahusika wakuu katika mchakato wa kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya watu. Wawe ni watu wenye matumaini kwa kukazania mambo msingi katika maisha.

Baba Mtakatifu anaiomba Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala, ili aweze kuambatana na vijana, kwa kuwasaidia kama anavyoweza na kuwekeza katika majiundo makini dhidi ya mwelekeo unaotaka kuwasukumizia pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.