2015-04-20 16:08:00

Prof. E.Toaff alikuwa ni kiongozi mwadilifu na chombo cha majadiliano


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Professa Elio Toaff, Rabbi mstaafu wa Roma aliyefariki dunia Jumapili tarehe 19 Aprili 2015 na kuzikwa mjini Livorno, Kaskazini mwa Italia tarehe 20 Aprili 2015. Baba Mtakatifu amemwandikia salam hizi za rambi rambi Dokta Riccardo di Segni, Rabbi mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma.

Baba Mtakatifu anamkumbuka Marehemu Rabbi Toaff, kiongozi maarufu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma. Ni kiongozi aliyejipambanua katika historia ya Wayahudi nchini Italia na mchango wao katika ustawi na maendeleo ya Italia. Katika maisha yake, alibahatika kuwa ni kiongozi mwenye mvuto kutokana na maadili yaliyokuwa yanajikita katika undani wa binadamu.

Baba Mtakatifu anamkumbuka Marehemu Rabbi Toaff  kutokana na moyo wake wa ukarimu na uwajibikaji katika ukweli na uwazi; kwa kujifunga kibwebwe kuendeleza majadiliano ya kidini na mahusiano mema kati ya Wakristo na Wayahudi, kiasi cha waamini wa dini hizi mbili kushuhudia tukio la kihistoria lililomkutanisha na Mtakatifu Yohane Paulo II kwenye Sinagogi la Roma. Baba Mtakatifu anapenda kumtolea Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma, mapendo na uaminifu, sala na maombi yake, ili aweze kumpokea Marehemu Rabbi Toaff kwenye ufalme wake wa amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.