2015-04-20 14:39:00

Misimamo mikali ya imani inatishia: amani, umoja na mfungamano wa watu


Baraza la Marabbi kutoka Ulaya katika mkutano wao wa kwanza na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2015 wamegusia kwa namna ya pekee uhuru wa kuabudu na mashambulizi ya kidini yanayofanywa na watu wenye misimamo mikali ya imani, kiasi cha kutishia amani, usalama na maendeleo ya wengi. Mkutano huu umefanyika wakati ambapo Kanisa linajiandaa kuadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu majadiliano ya kidini “Nostra Aetate”.

Hivi karibuni, Jumuiya za Kiyahudi zimekuwa pia ni walengwa wakuu wa mashambulizi kutokana na misimamo mikali ya kiimani, hali inayotishia uhuru wa kuabudu. Baraza la Marabii kutoka Ulaya limeipongeza Vatican kwa kuendelea kujikita katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani. Misimamo mikali ya kiimani ni hatari kwa amani na mfungamano wa kimataifa. Marabbi wamemwomba, Baba Mtakatifu kusaidia mchakato wa ujenzi wa madaraja yatakayowaunganisha watu kutoka Mashariki na Magharibi, ili kwa pamoja waweze kuwa ni wajenzi wa amani Barani Ulaya na ulimwenguni kote. Baraza la Marabbi limemtakia Baba Mtakatifu baraka na amani katika maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.