2015-04-20 11:46:00

Majadiliano ya kidini: Ukuu wa Mungu na utakatifu wa maisha!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na Baraza la marabbi kutoka Ulaya waliomtembelea mjini Vatican. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa salam zake za rambi rambi kutokana na kifo cha Elio Toaff  Rabbi mkuu mstaafu wa Roma, kilichotokea, Jumapili jioni tarehe 19 Aprili 2015. Anaungana na Jumuiya ya Kiyahudi inayoomboleza msiba huu mzito kwani Rabbi mstaafu Toaff alikuwa ni mtu wa amani aliyekita maisha yake katika majadiliano ya kidini. Haya ni majadiliano ambayo yanaendelezwa na Mama Kanisa tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu majadiliano ya kidini, unaojulika kama Nostra aetate, ambao tarehe 28 Oktoba, 2015, Kanisa litaadhimisha miaka 50 tangu kuchapishwa kwake.

Huu ni Waraka rejea katika majadiliano ya kidini, ambao umeliwezesha Kanisa kuona cheche za mafanikio katika kudumisha urafiki na maridhiano katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita hususan katika medani mbali mbali za maisha. Kutokana na mawazo mepesi mepesi na tabia ya ukanamungu, watu wanaanza kuishi kana kwamba, hakuna Mungu na baadhi ya watu kutaka kuchukua nafasi ya Mungu, ili kudhibiti kila kitu kwa ajili ya mafao binafsi. Binadamu anapaswa kukumbuka kwamba, maisha yake ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayepaswa kuaminiwa sanjari na kukuza maana ya dini katika maisha ya mwanadamu. Binadamu hana budi kushuhudia Utakatifu wa Mungu na maisha ya binadamu na kwamba, maisha ni kito cha thamani kubwa sana.

Baba Mtakatifu anaonesha masikitiko yake kutokana na kuongezeka kwa madhulumu, nyanyaso na chuki za kidini dhidi ya Wayahudi. Kanisa linapenda kuonesha mshikamano wa dhati na Wayahudi kwa kutambua mateso na mahangaiko waliyokumbana nayo, lakini kwa namna ya pekee, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kufungwa kwa kambi ya mauaji ya Auschwitz, ambako Wayahudi wengi walipoteza maisha yao. Hili ni onyo kali kwa vijana wa kizazi kipya na kile kijacho, ili kuondokana na vitendo vya nyanyaso, dhuluma na chuki za kidini dhidi ya Wakristo au waamini wa dini nyingine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.