2015-04-20 09:27:00

Jubilee ya miaka 200 ya kuzaliwa Don Bosco: Onesho la Sanda Takatifu!


Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia, Jumapili tarehe 19 Aprili 2015 limezindua rasmi Onesho la Sanda Takatifu, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco, mtume wa Vijana. Tukio hili linaongozwa na kauli mbiu “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko kuu” na limezinduliwa rasmi na Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Jimboni humo ili kutoa heshima yake kwenye Sanda Takatifu wakati wa hija yake ya kitume Jimboni humo kuanzia tarehe 20 hadi 21 Juni 2015.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Cesare Nosiglia anabainisha kwamba, Yesu Kristo mfufuka ni chemchemi yenye nguvu ya kuweza kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha katika familia, maeneo ya kazi na katika maisha ya kijamii kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa. Kuanzia tarehe 19 Aprili hadi tarehe hadi tarehe 24 Juni 2015, waamini na watu wenye mapenzi mema watafanya hija ya imani, ili kuangalia alama za mateso ya Kristo zinazoonekana kwenye Sanda Takatifu, taswira ya Injili kama alivyobainisha Mtakatifu Yohane Paulo II.

Hiki ni kielelezo cha upendo mkuu unaofumbata huruma ya Mungu, changamoto ya kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo unaoguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani. Sanda Takatifu ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu, mwaliko kwa waamini kuonesha kweli moyo wa shukrani na kwamba, huruma yake ni kubwa zaidi kuliko hata mapungufu ya kibinadamu. Mwanadamu kadiri ya mpango wa Mungu amepewa dhamana ya kulinda na kutunza kazi ya uumbaji dhidi ya ubinafsi, uchoyo na hali ya kutojali wala kuguswa na mahaiko ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wajifunze kushinda ubaya kwa kutenda mema sanjari na kuendeleza mchakato wa haki, amani na upatanisho; tunu msingi zinazojikita katika haki, ukweli na upendo.

Askofu mkuu Nosiglia anasema, Onesho la Sanda Takatifu ya Yesu Kristo mteswa, iwe ni fursa kwa waamini kuguswa na upendo wa Mungu, ambaye hakusita kumtoa Mwanaye wa pekee ili ateswe na kufa Msabani na siku ya tatu kufufuka kutoka wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu. Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mashahidi wa tukio hili, linalowakumbusha matukio ya Ijumaa kuu kuelekea Pasaka ya Bwana, ili kuweza kuwafunulia binadamu upendo wa Mungu unaokoa na kuponya. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni mashuhuda amini wa Fumbo la Pasaka, kwa njia ya matendo ya huruma yanayoibua matumaini mapya miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.