2015-04-19 13:45:00

Wakristo wanaalikwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka!


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 19 Aprili 2015, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda wa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Kwa mwamini aliyekutana na Yesu katika maisha yake, kamwe hawezi kuficha mang’amuzi haya na kwa njia ya wafuasi wake, Yesu anataka ukweli kuhusu Fumbo la Ufufuko liweze kuwafikia watu wengi zaidi. Mama Kanisa anaendeleza dhamana na utume huu katika nyakati, changamoto kwa kila Mkristo kuhakikisha kwamba, kweli anakuwa ni shuhuda wa Kristo Mfufuka anayeendelea kuwa kati ya watu wake.

Baba Mtakatifu anasema, shuhuda ni mtu aliyeona, anayekumbuka na kusimulia; mambo msingi yanayofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mtu ambaye ameona na kuguswa na mang’amuzi haya katika hija ya maisha yake; anasimulia yale mambo msingi yaliyomwezesha kubadili mwelekeo wa maisha yake. Ushuhuda wa Mkristo ni ujumbe wa Wokovu unaojikita katika maisha na utume wa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Waamini wanaweza kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka kwa njia ya sala na hija inayotekelezwa na Mama Kanisa kwa kufumbatwa katika msingi wa Sakramenti ya Ubatizo, inayorutubishwa kwa Ekaristi Takatifu na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara; inayomwezesha mwamini kuendeleza hija ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni hija inayoongozwa na Neno la Mungu, kumbe, kila Mkristo anaweza kuwa ni shuhuda wa Kristo Mfufuka kwa njia ya maisha yanayojikita katika tunu msingi za Kiinjili, furaha, ujasiri, wema, amani na huruma. Kamwe Wakristo wasikubali kumezwa na malimwengu, ubatili wa maisha na ubinafsi, bali wadhihirishe ile nguvu ya Kristo inayookoa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.