2015-04-19 13:59:00

Kuna umati mkubwa wa wahamiaji umekufa maji Baharini Mediterrania


Mara baada ya tafakari ya Sala ya Malkia wa mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 19 Aprili 2015, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha masikitiko yake kutokana na taarifa zinazoendelea kusikika kwamba, kuna umati mkubwa wa wahamiaji umezama na kufa maji ufukweni mwa Libia. Anapenda kuwahakikishia ndugu na jamaa walioguswa na msiba huu mzito uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Anaiomba kwa namna ya pekee, Jumuiya ya Kimataifa kuishughulikia changamoto hii kwa nguvu zaidi ili kusalimisha maisha ya watu wanaoendelea kufa maji kila siku kwenye Bahari ya Mediterrania.

Baba Mtakatifu anasema, hili ni kundi la watu ambao wanakumbana na vita, nyanyaso na madhulumu mbali mbali; ni watu wanaotafuta nafuu na furaha ya maisha. Kutokana na uchungu huu mkubwa, Baba Mtakatifu amewaomba waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuwaombea wahamiaji hawa. 

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa makundi mbali mbali ya waamini na mahujaji kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Roma. Anaunga mkono juhudi zinazofanywa na waandamanaji kutoka Jimbo Kuu la Varsavia, katika kulinda na kutetea utakatifu wa maisha. Ametambua uwepo wa kundi la wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, kinachoadhimisha Siku yake ya 91, tarehe 19 Aprili 2015. Anawataka wanafunzi kuendeleza mchakato wa malezi na majiundo makini kitamaduni, huku wakijitahidi kuunganisha imani na sayansi; maadili na taaluma.

Baba Mtakatifu mwishoni, amekumbusha kwamba, Jimbo kuu la Torino, Jumapili tarehe 19 Aprili 2015 limezindua Onesho la Sanda Takatifu. Ni matumaini yake kwamba, panapomajaliwa hapo tarehe 21 Juni 2015 ataweza kuungana na waamini wengine kutoa heshima yake kwa Sanda takatifu, ili hatimaye, kuweza kuuona uso wa Yesu unaonesha huruma ya Mungu kwa kutambua ndani mwake watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.