2015-04-18 09:41:00

Siku ya kuombea miito duniani: Vijana itikieni wito wa Upadre na Utawa


Changamoto kubwa ambayo inalikabili Kanisa kwa wakati huu si "uhaba wa Mapadre bali uvivu wa vijana kuitikia wito wa kuijiunga na miito mitakatifu", kwani Mwenyezi Mungu daima anaendelea kuwaita watu kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, lakini kwa bahati mbaya, wengi wao, bado hawana ari na mwamko wa kuweza kuitikia sauti hii ya Mungu kwa moyo wa ujasiri. Wito unapobaki bila kupewa jibu makini, linakuwa kweli ni jambo la kusikitisha.

Hii ni changamoto inayotolewa na Askofu Mark O’Toole wa Jimbo la Playmouth, Uingereza kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya 52 ya kuombea miito duniani, inayoadhimishwa, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo mchungaji mwema. Waamini kwa namna ya pekee, wanahamasishwa kujisikia kuwa ni sehemu ya mpango wa Mungu na kwamba, wanaitwa ili kutoa huduma makini kama mtu wa ndoa, au Padre au Mtawa au hata wakati mwingine kuishi maisha ya kawaida kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Askofu Mark anasema kwamba, Mwenyezi Mungu analijalia Kanisa karama, neema na baraka zote linalohitaji, ili kutekeleza dhamana na utume wake kwa Watu wa Mataifa. Hii ni changamoto kwa wazazi na walezi kuwasaidia watoto wao kuwa na mwelekeo mpana na wakarimu kwa Kanisa pale watoto wao wanapoonesha ni ana hamu ya kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani. Vijana wa kizazi kipya wasaidiwe na kuwezeshwa si tu kuwa mabingwa katika taaluma, bali pia kwa kuitikia miito mitakatifu ili waweze kuwa watakatifu na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wake.

Waamini wanakumbushwa kwamba, utakatifu wa maisha ni changamoto kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, wawe wanaishi katika maisha ya ndoa, huko wanapaswa kusaidiana na kutakatifuzana. Kwa mapadre na watawa, maisha, wito na huduma kwa Familia ya Mungu iwe ni chachu ya kukoleza utakatifu wa maisha. Waamini wanaweza kujikita pia katika huduma ya Neno la Mungu na kwa Familia ya Mungu kwa njia ya Darala la Ushemasi wa kudumu. Kwa njia ya sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wanahamasishwa kuwa ni watakatifu kama Baba yao wa Mbinguni alivyo mtakatifu.

Askofu O’Tool anabainisha kwamba, bila Mapadre, hakuna Kanisa wala Sakramenti. Kumbe, wito wa Upadre na maisha ya kitawa ni mwaliko wa pekee kwa baadhi ya waamini kujisaka kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake. Kwa njia ya mashauri ya Kiinjili, Mapadre na Watawa wanakuwa ni kielelezo cha sadaka, kwa ajili ya wengi, tunu ambazo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia zinakabiliana na changamoto nyingi.

Vijana wanaojisikia kwamba, wameitwa na Mungu katika maisha ya Upadre na Utawa hawana sababu ya kuogopa, bali wajitokeze kifua mbele tayari kujibu wito na mwaliko huu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mapadre ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kuitikia wito wa kipadre na maisha ya kitawa, kuwaombea na kuwasaidia Mapadre na Watawa kuweza kutekeleza maisha na wito wao kwa amani na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.