2015-04-18 15:03:00

Rais Sergio Mattarella wa Italia akutana pia na Kardinali Parolin


Rais Sergio Mattarella wa Italia, tarehe 18 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican na baadaye amekutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekua ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Taarifa inabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake, Rais Sergio Mattarella wameridhika na mauhusiano mazuri yaliyopo kati ya Vatican na Italia na kwamba, Nchi hizi mbili zinaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi hususan katika itifaki ya masuala ya fedha; mkataba uliotiwa sahihi hivi karibuni na pande hizi mbili. Viongozi hawa wamejadili kwa kina na mapana masuala ya kijamii na kiuchumi yanayotikisa maisha ya wananchi wengi wa Italia, lakini zaidi kuhusiana na: tunu msingi za maisha ya kifamilia, elimu, ajira na changamoto ya wahamiaji.

Viongozi hawa wamepongeza ushirikiano wa dhati unaofanywa kati ya Kanisa na Serikali ya Italia katika medani mbali mbali za maisha, hususan miongoni mwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wametupia jicho pia katika masuala ya kimataifa na kwa namna ya pekee, vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia bila kusahau majanga yanayoendelea kuwakumba wahamiaji kutoka Afrika ya Kaskazini, wanaokufa maji kila kukicha. Vaticana na Italia wameonesha utashi wa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi katika masuala ya kimataifa, hususan katika kulinda na kutetea uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.