2015-04-17 15:15:00

WCC: Hakuna sababu za kisiasa wala kimaadili zinazohalalisha vita!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini, hivi karibuni limehitisha mkutano wa ushauri kwa ajili ya kutafuta amani nchini Sudan ya Kusini, mkutano ambao umefanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia na kuhudhuriwa na viongozi wa Makanisa nchini Sudan ya Kusini. Kanisa limeamua kuendeleza mchakato wa kutafuta amani baina ya Serikali na Kikundi cha upinzani baada ya pande hizi mbili kuonesha hali ya kutoaminiana. Umekuwa ni mkutano ambao umegusia mahitaji msingi ya wananchi wa Sudan ya Kusini sanjari na kuonesha umuhimu wa kuwa na jukwaa pana zaidi linaloweza kujadili hatima ya maisha ya wananchi wa Sudan ya kusini kwa uhuru zaidi.

Baraza la Makanisa katika kipindi hiki cha Pasaka, linaialika Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, kuanza mchakato wa  maisha mapya kwa kujikita katika Fumbo la Ufufuko, ili kuondokana na chachu ya mambo ya kale iliyosababisha kinzani na vita, ili kuanza tena mchakato wa uponyaji na upatanisho wa kitaifa. Bado watu wanaendelea kuuguza makovu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan. Kuna ukosefu mkubwa wa utawala wa sheria na kwamba, Serikali inaonekana kana kwamba iko likizo, kiasi cha watu kujichukulia sheria mikononi mwao pamoja na kulipiza kisasi.

Kadiri vita inavyoendelea kurindima nchini humo, ndivyo itakavyokuwa vigumu kung’oa ndago za utamaduni wa kifo. Watu wanakosa amani na usalama wa maisha yao na kwamba, ukabila unaendelea kupamba moto na kuvunjilia mbali umoja na mshikamano wa kitaifa. Mapigano na usajili wa askari wapya unaendelea, hali ambayo inatishia usalama na amani Sudan ya Kusini.

Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni  anasema kwamba, umefika wakati wa kuleta amani na maridhiano Kusini mwa Sudan na kwamba, viongozi wa Makanisa wanataka amani, ustawi na maendeleo ya wananchi wote. Kwa muda wa miaka 40 Baraza la Makanisa limefanya hija ya kiroho pamoja na Familia ya Mungu nchini Sudan ili kuhakikisha kwamba, haki na amani ya kweli vinatawala. Hakuna sababu ya msingi wala kimaadili ya kuendeleza vita, kinzani na migawanyiko Kusini mwa Sudan.

Vita isitishwe, viongozi waanze mchakato wa majadiliano katika ukweli, amani na utulivu. Viongozi wa Makanisa ni mabalozi wa amani na wametumwa ili kuwapatanisha wananchi wa Sudan ya Kusini. Haki na amani ni fadhila ambazo zinapaswa kuwaongoza wananchi wa Sudan ya Kusini. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linatarajia kuitisha siku maalum ya sala kwa ajili ya kuombea amani, utulivu na maridhiano Sudan ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.