2015-04-17 11:42:00

Mwaka wa Watawa Duniani: Watawa na majadiliano ya kidini na kitamaduni


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali kwani hii ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaopania kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume nchini Hispania, Confer, kwa kutambua umuhimu wa maisha na utume wa watawa katika kukoleza majadiliano ya kidini, kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 19 Aprili, 2015 linaendesha kongamano la kitaifa ili kuangalia changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo mintarafu Waraka wa “Nostra Aetate” uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na majadiliano ya kidini.

Hii ni nafasi ya kukutana na kujadiliana na watu kutoka katika tamaduni, mila, desturi na dini mbali mbali kwa lengo la kuimarisha misingi ya haki, amani na utulivu. Majadiliano haya yanalenga pia kukoleza moyo wa upendo, udugu na ukarimu hasa kwa wageni na wahamiaji ambao wengi wao wanahudumiwa na Mashirika ya kitawa na kazi za kitume. Mama Kanisa nafanya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Waraka wa “Nostra Aetate ulipochapishwa na tangu wakati huo kumekuwepo na changamoto mbali mbali katika kukoleza majadiliano ya kidini.

Watawa wakati huu wanaangalia mambo msingi yaliyopelekea kutungwa kwa waraka huu na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Watawa wanapembua kwa kina na mapana ili kuangalia mchango wanaoweza kuutoa katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni. Ni wakati wa kusali na kutafakari pamoja na kushirikishana mang’amuzi, fursa na changamoto za majadiliano ya kidini katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.