2015-04-17 13:58:00

Mwaka wa Familia Jimbo kuu la Mwanza: Shuhudieni Injili ya Uhai!


Askofu mkuu Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika barua yake ya kichungaji katika maadhimisho ya Mwaka wa Familia Jimbo kuu la Mwanza anawataka waamini kufanya hija za maisha ya kiroho kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha imani yao na kama kielelezo cha sadaka katika maisha. Leo katika Makala haya, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kama sehemu ya mchakato wake wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015 inakuletea sehemu ya barua hii kwa kujikita katika hija na umuhimu wa waamini kusimama kidete kulinda na kutangaza Injili ya Uhai na Familia.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anawahimiza waamini kufanya hija kwa ajili ya kusali ili kuabudu, kuomba, kuomba na kufanya toba, ili kutafuta msamaha wa dhambi sanjari na kuonja huruma ya Mungu. Hija ni kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake; ni sadaka na majitoleo yanayooneshwa na waamini.

Kwa namna ya pekee, waamini wanaalikwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Uhai kwani Mwenyezi Mungu ndiye aliye hai na asili ya uhai wote na kwamba, Familia ni kitalu ambamo uhai unasitawishwa na kuendelezwa. Waamini wanahamasishwa kupinga utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba, kwa kuimarisha malezi makini kwa vijana, kwa kuondokana na imani za kishirikina pamoja kutafuta kazi halali ya kujipatia kipato.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anawahimiza kwa namna ya pekee madaktari na wahudumu katika sekta ya afya, kuzingatia kanuni maadili ya taaluma ya tiba na kwamba, wajisadake zaidi katika kudhibiti utamaduni wa kifo unaoisakama jamii ya binadamu kwa nyakati hizi. 








All the contents on this site are copyrighted ©.