2015-04-17 08:01:00

Muafaka umefikiwa kati ya Wakuu wa Mashirika ya kitawa na Baraza!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 16 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Wakuu wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Marekani, Lcwr, ambalo kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2012 lilikuwa linafanyiwa uchunguzi na Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa. Katika mkutano huu, pande zote mbili zimefikia muafaka na kutoa tamko la pamoja baada ya tathmini ya kina kuhusu usahihi wa mafundisho ya Kanisa kufanywa na Baraza la Kipapa na kutolea maamuzi.

Kwa kipindi cha miaka minne, pande hizi zimeshirikiana kwa pamoja ili kuandika Katiba mpya ya Shirikisho la Mashirika ya Kitawa nchini Marekani, umuhimu wa kuwa makini katika machapisho yanayotolewa na watawa, majiundo ya kina kwa wawezeshaji wakuu wa Shirikisho hili pamoja na kubainisha vigezo vinavyoweza kutumika kwa ajili ya kuwachagua wasemaji wakuu wa mashirika ya kitawa na kwa maneno machache, changamoto nyingi zimejadiliwa na kupewa maamuzi ya kina, ili kujenga na kudumisha utume na maisha ya kitawa mintarafu mafundisho ya Kanisa.

Taarifa ya pamoja imewasilishwa mjini Vatican wakati viongozi wakuu wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume walipokutana na kuzungumza na Kardinali Gerhard Muller, mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa na baadaye, wakakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha na utume wa Shirikisho hili, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani.

Ni matumaini ya Kardinali Muller kwamba, Shirikisho hili litaendelea kutambua na kujikita katika maisha na utume wake, ili kuyasaidia Mashirika ya kitawa na kazi za kitume nchini Marekani kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake mintarafu Mapokeo ya Kanisa. Wakuu wa Shirikisho hili wanasema wamefurahi kuhitimisha uchunguzi huu ambao umewasaidia kupata mwanga mpana zaidi kuhusu mwono na matumaini ya maisha na utume wa watawa hasa katika masuala nyeti sanjari na utekelezaji wake.

Uchunguzi na majadiliano haya yamefanyika katika hali ya upendo na udugu, hekima na busara pamoja na sala. Kwa pamoja wametambua: dhamana, wajibu na matumaini ya watu wanaowahudumia kwa njia ya Mashirika ya kitawa. Kwa pamoja wametambua kwamba, kuna mambo mengi msingi yanayowaunganisha, kuliko yale machache ambayo yalikuwa yanataka kuwagawa na kuwatenganisha. Itakumbukwa kwamba, Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa lilikuwa limebainisha “matatizo makubwa na mazito mintarafu mafundisho tanzu ya Kanisa” yaliyokuwa yameonekana katika maisha na utume wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume nchini Marekani.

Kimsingi, baadhi ya mada ambazo zilikuwa zinaleta msuguano ni pamoja na: Daraja takatifu kwa wanawake, sera na mikakati ya huduma za kichungaji kwa watu wanaoishi katika ndoa za jinsia moja; misimamo mikali kuhusu wanawake kinyume cha Mafundisho na Mapokeo ya Kanisa. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyopelekea majadiliano ya kina kati ya Maaskofu nchini Marekani, Watawa pamoja na Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa na kwamba, majadiliano haya hayana budi kudumishwa na kuendelezwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa nchini Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.