2015-04-17 08:26:00

Janga la Ebola limedhibitiwa, lakini wasi wasi ni machafuko ya kisiasa


Baraza la Maaskofu Katoliki Sierra Leone linabainisha kwamba, janga la Ebola limesababisha madhara makubwa kwa maisha na ustawi wa wananchi wengi Afrika Magharibi. Zaidi ya watu elfu kumi na mbili waliambukizwa ugonjwa wa Ebola na kati yao wagonjwa 2, 900 walifariki dunia. Wananchi wengi bado wanaogopa na wana wasi wasi mkubwa kuhusu usalama wa maisha yao. Katika kipindi hiki cha Pasaka, Baraza la Maaskofu linawataka waamini kujenga imani na matumaini kwa Yesu Kristo Mfufuka, tayari kusonga mbele katika utekelezaji wa majukumu yao yak ila siku.

Baraza la Maaskofu Katoliki Sierra Leone linabainisha kwamba, baada ya ugonjwa wa Ebola kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa, lakini kwa sasa, wasi wasi mkubwa unaanza kuonekana kutokana na kinzani za kisiasa, mambo yanayoweza kuhatarisha misingi ya haki, amani, ustawi, mshikamano na umoja wa kitaifa. Kinzani za kisiasa ni jambo ambalo halina budi kupewa kipaumbele cha pekee, ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa. Wananchi wasimame kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na kwamba ustawi na maendeleo ya Sierra Leone yako mikononi mwao. Wanawajibika kudumisha demokrasia ya kweli, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, ili hatimaye, kuwa na uongozi thabiti unaojipambanua kwa jili ya mafao ya wengi.

Maaskofu Katoliki Sierra Leone, wanaitaka Familia ya Mungu nchini humo, kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa sanjari na kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola, kwa kuheshimu protokali zilizowekwa na wizara ya afya ili kulinda wanawanchi. Kuna haja pia kwa wananchi kuheshimu utawala wa sheria na kutafuta haki zao msingi kisheria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.