2015-04-16 11:10:00

Wakenya: shikamaneni katika misingi ya haki, amani na upatanisho!


Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa jimbo kuu la Mombasa, Kenya, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, shambulizi la kigaidi lilofanywa na kikundi cha Al Shabaab na kusababisha vifo vya wanafunzi 148 kutoka Chuo kikuu cha Garissa ni kilele cha chuki na uhasama unaopandikizwa na baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kidini. Ni ubaguzi unaojikita katika katika mizizi ya kidini, jambo ambalo ni hatari sana kwa umoja, mshikamano na mfungamano wa wananchi wa Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa wale wote ambao wanaendelea kuguswa na kutikishwa na mikasa hii katika maisha. Maaskofu wakati huu wa hija yao ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican wanaikumbuka na kuiombea Familia ya Mungu nchini Kenya, ili iweze kujikita katika misingi ya haki, amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anasema wananchi wa Kenya wanapaswa kuthamini na kujivunia tofauti zao za kidini, kikabila na kisiasa kama utajiri na amana kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha yao, changamoto ya kuzitumia fursa zote hizi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi na kamwe zisiwe ni chanzo cha kinzani na migawanyiko kwa misingi ya udini, ukabila au siasa, kwani furaha ya upinde wa mvua ni rangi zake saba!

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anabainisha kwamba, kuna changamoto nyingi ambazo zinaendelea kuwakabili wananchi wa Kenya katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano. Lakini wanakumbushwa kwamba, Yesu anawataka kubeba vyema Misalaba ya maisha yao na kisha kumfuasa kwa imani na matumaini na kwamba, Kristo yuko pamoja nao kama alivyoandamana na wafuasi wa Emmau ili kuwafafanulia Maandiko Matakatifu na kwamba, wanaalikwa kwa namna ya pekee kukinywea Kikombe cha mateso ya Kristo kwa njia ya mateso na mahangaiko yao ya kila siku.

Familia ya Mungu nchini Kenya inakumbushwa kwamba, yataka moyo kweli kweli kuwa Mkristo na kwamba, bado kuna changamoto nyingi katika maisha kama vile: misigano ya imani, matatizo na changamoto za maisha ya ndoa na familia; dhamana na majukumu mbali mbali ambayo imekabidhiwa kuyaendeleza. Lakini pamoja na changamoto zote hizi, Yesu bado anaandamana na wafuasi wake, hadi utimilifu wa dahali. Yesu ataendelea kuwa pamoja nao na kuwwatia shime katika magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira na wasi wasi katika maisha. Kwa wakati wake anasema Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde, Mwenyezi Mungu atawajibu na kuwafariji. Waendelee kusali kwa kuomba na kushukuru kwa mema mengi ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia katika maisha yao bila hata kustahili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.