2015-04-16 13:34:00

Papa mstaafu Benedikto XVI: anasherehekea Miaka 88 tangu alipozaliwa!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican siku ya Alhamisi, tarehe 16 Aprili 2015 ametolea nia maalum kwa ajili ya kumwombea Papa mstaafu Benedikto XVI anayeadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 88 ya maisha.Tangu alipong’atuka kutoka madarakani kwa hiyari yake mwenyewe, Papa mstaafu Benedikto XVI anaishi kwenye Monasteri ya “Mater Ecclesiae” iliyoko mjini Vatican, katika hali ya utulivu, tafakari, sala na kuendeleza kazi zake za kitaaluma. Huu ni uzee uliotukuka katika utulivu na heshima kuu pasi na makuu!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu amewaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuendelea kumsindikiza Papa mstaafu Benedikto XVI kwa sala, ili Mwenyezi Mungu aweze kumkirimia wingi wa afya njema, amani na utulivu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.