2015-04-16 07:16:00

Kanisa Katoliki Kenya: Mchakato wa Uinjilishaji wa kina


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linajiandaa kuadhimisha Jubilee ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari nchini humo, sanjari na kumtangaza Mtumishi wa Mungu Irene Stefani, aliyekuwa anajulikana kwa wakati huo kama Aurelia Jacoba Maria Mercedes wa Shirika la Watawa Wamissionari wa Consolata kuwa Mwenyeheri.

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu hapo tarehe 23 Mei 2015, Jimboni Nyeri, ili kumtangaza Mtumishi wa Mungu Irene Stefani kuwa Mwenyeheri. Hili ni tukio la pekee kabisa nchini hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, ili kuwaonjesha walimwengu sadaka na mchango wa watawa katika maisha na utume wa Kanisa.

Taarifa zinaonesha kwamba, Mwezi Mei, Kanisa Katoliki nchini Kenya litafanya kumbu kumbu ya miaka 110 tangu kulipofanyika mkutano wa kwanza wa kimissionari, uliopembua kwa kina na mapana matatizo, changamoto na fursa za kupandikiza mbegu ya Neno la Mungu katika maisha ya Familia ya Mungu nchini Kenya.

Ni katika mkutano huu kwamba, Wamissionari walijiwekea dira na mwongozo wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kwa kubainisha kwanza kabisa mihimili ya Uinjilishaji, uliotoa kipaumbele cha kwanza kwa Makatekista kutokana na ukweli kwamba, Mapadre na Watawa walikuwa ni wachache sana, ikilinganishwa na ukubwa wa eneo na idadi ya watu.

Wamissionari wakaamua kuwekeza katika elimu bora mashuleni kama sehemu ya mchakato wa mikakati ya Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; elimu ikawa ni nyenzo ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la ujinga na umaskini, tayari kuikumbatia huruma na upendo wa Mungu. Sekta ya afya, ilikuwa ni kipaumbele cha pili, kilichozingatiwa katika mchakato wa Uinjilishaji, ndiyo maana hata leo hii, Kanisa nchini Kenya ni mdau mkubwa wa huduma katika sekta ya afya, hasa vijijini.

Wamissionari waliamua kuwafuata waamini mahali walipokuwa licha ya magumu na changamoto ambazo wangekumbana nazo sanjari na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira. Leo hii Parokia nyingi zimezungukwa na maeneo ya kijani kibichi, yote hii ni mikakati ya Uinjilishaji na matunda yake yanaonekana hadi leo hii, mwenye macho haambiwi, tazama!

Kanisa Katoliki nchini Kenya linaadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani kwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kulipatia Mapadre wa zawadi ya imani, Fidei Donum, ambao kwa miaka hamsini wamechakarika usiku na mchana ili kuitangazia Familia ya Mungu nchini Kenya, Injili ya Furaha. Jubilee hii itaadhimishwa kwa kishindo, mwezi Julai, 2015. Tume ya Uinjilishaji wa Watu na Tume ya Kimissionari ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa pamoja zitaadhimisha Jubilee ya miaka 50 na 25 tangu kuanzishwa kwake.

Askofu mkuu Charles Balvo, Balozi wa Vatican  nchini Kenya, anayataka Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari kupembua kwa kina na mapana changamoto, matatizo na fursa za Uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kuweza kutoa majibu muafaka, kwa kutambua kwamba, nyakati hizi hali si lelemama, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita katika maisha na utume wa Kanisa. Mihimili ya Uinjilishaji katika historia na maisha ya Kanisa, daima imepambana na hatimaye, Injili ikasonga mbele.

Askofu John Oballa wa Jimbo Katoliki Ngong, Kenya anabainisha kwamba, mchakato wa Uinjilishaji wa kina hauna budi kujikita katika kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, hususan wale ambao bado hawajasikia Neno la Mungu likitangazwa masikioni mwao sanjari na  kuwaimarisha wale waliolisikia, lakini wakamezwa na  malimwengu kiasi cha kushindwa kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Kwa upande wake, Askofu Peter Kihara, anaitaka mihimili ya Uinjilishaji kujikita katika mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha inayojikita katika imani na mapendo; mambo yenye mvuto na mashiko katika ushuhuda wa Injili kwa watu wa nyakati hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA. 








All the contents on this site are copyrighted ©.