2015-04-15 07:29:00

Umoja wa Mataifa unawakumbuka wasichana 276 waliotekwa na Boko Haram


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anasema kwamba, mwaka mmoja umegota tangu wanafunzi 276 waliokuwa wanasoma katika shule ya Chibok, Borno, Kaskazini mwa Nigeria walipotekwa nyara na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram. Baadhi yao walibahatika kuwatoroka watesi wao, lakini hatima ya kundi kubwa la wasichana hawa bado haijulikani hadi leo hii. Jumuiya ya Kimataifa kamwe haipaswi kuwasahau wasichana hawa na kwamba, bado anaendelea kuwahimiza wateka nyara hao kuwaachia wasichana hawa ili waweze kujiunga na familia zao.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Boko Haram imezidisha mashambulizi yake dhidi ya raia wasiokuwa na hatia ndani na nje ya mipaka ya Nigeria. Kuna maelfu ya watoto na vijana ambao wamelazimika kuzikimbia familia na miji yao na hivyo kulazimika kuishi kama wakimbizi na wahamiaji na hivyo kunyimwa ile haki ya kuwa na amani na usalama; utu na heshima. Kumekuwepo na mauaji ya kinyama, utekaji nyara pamoja na kuwatumia watoto wadogo katika mashambulizi ya kujitosa mhanga; mambo ambayo yanasikitisha sana.

Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, mashambulizi dhidi ya taasisi za elimu ni uvunjwaji wa haki msingi za kibinadamu kimataifa. Wanafunzi wana haki ya kwenda shule ili kupata elimu, jambo ambalo linahitaji hali ya usalama na amani. Boko Haram inapaswa kushughulikiwa kadiri ya sheria za kimataifa na kwamba, haiwezi kuendelea kuhatarisha maisha ya wanafunzi nchini Nigeria. Umoja wa Mataifa unaendelea kuunga mkono jitihada za wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya Kikundi cha Boko Haram.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.