2015-04-15 06:37:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, ninakuletea kipindi tafakari Neno la Mungu Dominika ya III ya Pasaka mwaka B. Mama Kanisa anatualika akisema Kristo amefufuka, ameyashinda mauti na hivi anatangaza maisha mapya kwao wote watakaomwamini na kumfuata.

Katika somo la kwanza Mitume wanahubiri Habari Njema ya maisha mapya wakiwaalika watu watubu dhambi zao ili waweze kuyajongea maisha haya mapya. Mtume Petro anasema ni kweli kwamba Wayahudi walimwua Bwana kwasababu ya ubinafsi wao lakini kwakuwa Mungu ni maisha mapya, ni huruma isiyo na kipimo anatangaza huruma na msamaha. Kumbe wanaalikwa kutubu na kumwongokea Mungu. Mwaliko huu anaoutoa Mtume Petro ni kwa ajili yetu pia hivi leo, yaani kubadirisha maisha yetu na kuaanza maisha ya ufufuko, maisha ya furaha na upendo kwa watu wote.

Mtume Yohane anakazia fundisho la Mtume Petro akisema ni kwa njia ya Kristo tunapata ondoleo la dhambi. Ni kwa njia ya Kristo mfufuka tunapatanishwa na Mungu Baba. Anasonga mbele katika kufundisha akisema, kupatanishwa na Mungu kunaambatana na kushika amri za Mungu. Ni kwa njia ya amri za Mungu mtu aweza kudai kuwa anamjua Mungu na anampenda. Kinyume na hili ni uwongo usio na maelezo.

Kristo ni yuleyule jana, leo na daima anawatokea Mitume kwa sababu anawapenda na anawapatia amani lililo tunda la Pasaka akisema “Amani kwenu”. Mitume hawa wanapopewa amani na Bwana wanashangaa na kuogopa. Wanadhani ni mzuka katikati yao. Hali ya kushangaa na kuogopa katika Neno la Mungu yatufundisha mvuto kuelekea mambo ya kimungu, mambo ya mbinguni, mambo matakatifu. Bikira Maria anapotokewa na Malaika Gabriel anashangaa na kuwa na woga! Vivyo hivyo Elizabeth mama yake Yohane Mbatizaji anapotembelewa na Mama wa Mungu anashangaa! Ni kweli mbele ya mafumbo matakatifu lazima kushangaa na kuwa na woga uliojaa imani ili kuzamisha mafumbo hayo ndani mwetu na kisha kuzaa matunda ndiyo matumaini na mapendo.

Mpendwa msikilizaji, katika mtiririko wa kushangaa Mitume nao wanapatwa pia na mashaka yakiambatana na mshangao, jambo hili pia lina maana katika Biblia! Linatoa nafasi ya kuanza safari ya imani polepole. Zipo sehemu mbalimbali katika Biblia ambapo Mitume na wanafunzi wengine wana mashaka. Kumbuka Mtume Petro akiwa pale Tiberia akivua samaki anapotokewa na Bwana anaona shaka. Fikiria juu ya wale wanafunzi wa Emmaus wanapotokewa na Bwana wanaona mashaka. Kuwa na  mashaka kifalsafa ni mwanzo wa hekima na hivi kiteologia mashaka hutuingiza polepole katika safari ya imani yaani kusadiki ufufuko wa Bwana ambao ndicho kilele cha imani yetu.

Mpendwa, nasi mara kadhaa tuna mashaka, Je, mashaka haya ni kwa ajili ya kuzamisha imani yetu katika kilindi cha Yesu Kristo mfufuka? Kama mashaka yatupeleka katika kilindi cha Yesu mfufuka basi tukaze mwendo daima ili kukomaa polepole katika safari hiyo ya imani na matumaini. Bwana anapowatokea wanafunzi wake anapata chakula pamoja nao, hili latufundisha, ingawa alikufa na kufufuka Yesu ni yuleyule jana, leo na daima.

Mpendwa, mwaliko kwetu kama tulivyosikia katika somo la kwanza ni toba kama mlango wa imani, mlango wa kumjua Mungu na mlango wa upendo kwa wanadamu. Basi shirikini furaha ya Pasaka ukichuchuchumilia toba na wongofu wa ndani na wa kweli, na hapo ndipo kuna maisha na ufuasi kwa Bwana hata kukitokea mashaka basi mashaka hayo yatapotea katika kukua kiimani na kifadhila tukimwelekea Kristu mkombozi wetu.

Ninakutakieni heri na baraka tele katika Dominika hii na zote zijazo, ukajazwe na Roho wa Mungu ili upate daima kuwa mtu wa toba na mapendo kwa jirani. Tumsifu Yesu Kristo. Kutoka Studio za Radio Vatican ni Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.