2015-04-15 14:05:00

Kardinali Tucci, SJ: Kiongozi mahiri aliyejisadaka kwa ajili ya Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko amepokea habari za msiba wa Kardinali Roberto Tucci, SJ., kwa masikitiko na majonzi makubwa na kwamba, anamwomba, Padre Adolfo Nicolas Panchon, Mkuu wa Shirika la Wayesuit kumfikishia salam zake za rambi rambi kwa wanashirika, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu mzito. Baba Mtakatifu Francisko anakumbuka mchango mkubwa uliotolewa na Kardinali Roberto Tucci enzi ya uhai wake. Aliwahi kuwa mkurugenzi mkuu wa Jarida la Wayesuit, maarufu kama “Civiltà Cattolica; mjumbe mtaalam wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican; Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican na kwa namna ya pekee mratibu wa safari za kitume za Khalifa wa Mtakatifu Petro nje ya Italia.

Baba Mtakatifu anasema, Kardinali Tucci anaacha urithi mkubwa wa huduma na ukarimu wa maisha ya kitawa yaliyosadakwa kwa ajili ya utume wa Kanisa, daima akijitahidi kuangalia mahitaji ya jirani na Kanisa. Alikuwa ni kiongozi mwaminifu kwa Injili na Kanisa la Kristo, akajitahidi kufuata mfano wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola.

Baba Mtakatifu anasema wakati huu anapenda kuinua sala zake kwa ajili ya kumwombea Marehemu Kardinali Roberto Tucci, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumpokea katika amani na furaha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia baraka zake za kitume kama alama ya mshikamano wa dhati na Shirika zima, wakati huu wa maombolezo wa kifo cha Kardinali Roberto Tucci.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.