2015-04-14 11:46:00

Mwaka wa Watawa Duniani: mkazo: upendo unaomwilishwa katika jumuiya!


Kwa njia ya Mashauri ya Kiinjili, watawa wanachangamotishwa na Mama Kanisa kushuhudia unabii wao katika maisha na utume wa Kanisa; mdano na kielelezo cha upatanisho haki na amani na kwamba, inawezekana watu kutoka katika makabila, lugha na mataifa mbali mbali kuishi kwa umoja, amani na upendo unaofumbatwa na Kristo kwa Kanisa lake. Muungano huu wa maisha ya upendo na udugu unaimarishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Kwa njia ya karama na mapaji mbali mbali, watawa wanaweza kuendelea kulipamba Kanisa, kwa kuwa waaminifu kadiri ya karama za waanzilishi wa mashirika yao ya kitawa na kazi za kitume. Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni kielelezo cha huduma makini inayomwlishwa katika maisha ya kimissionari, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, hususan miongoni mwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, Baba Mtaakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha watawa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Watawa wanapaswa kujikita katika majiundo makini ya awali na endelevu ili kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu wanaowazunguka.

Sr. Maria Marximilliana Massawe wa Shirika la Bikira Maria Immakulata anayefanya utume wake mjini Roma anasema, katika maisha yake ya ujana alivutiwa zaidi na upendo wa Mungu, ndiyo maana akaamua kujiunga na maisha ya kitawa, tayari kuwashirikisha wengine upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa. Upendo wa maisha ya kitawa kwa namna ya pekee kabisa unamwilishwa katika maisha ya kijumuiya, kwani Jumuiya si tatizo, linalohitaji ufumbuzi, bali ni Fumbo linalopaswa kumwilishwa kila siku ya maisha, kwa kupokeana na kusaidiana katika hija ya maisha ya kila siku.

Sr. Marximilliana anasema kwamba, Shirika lake katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, wamejiwekea mkakati wa kuhakikisha kwamba, wanajitoa zaidi na zaidi katika maisha na utume wa Shirika ndani ya Kanisa kwa kuonesha upendo wa dhati kwa Kristo na Kanisa lake na kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Sr. Marximilliana Massawe anakazia kwamba, kama Shirika, wamejiwekea malengo ya kuboresha maisha yao ya kijumuiya na kujitahidi kuishi kama ilivyokuwa kwa Jumuiya ya kwanza ya waamini, waliokuwa na moyo mmoja na roho moja, wakasaidiana kwa hali na mali. Mwenyezi Mungu amewakirimia watawa karama na mapaji mbali mbali ambayo wanapaswa kuyamwilisha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Shirika, Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Kwa njia hii, watawa wa Shirika la Bikira Maria Immakulata, watakuwa wanamwilisha upendo na kuushuhudia katika maisha ya kijumuiya, changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, mahali ambapo ubinafsi unatawala zaidi na watu kutaka kujitafuta wenyewe! Watawa wawe ni mfano wa upendo shirikishi unaomwilishwa katika maisha ya kijumuiya na kazi za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.