2015-04-13 15:16:00

WCC: Amani na upatanisho wa kweli ni mambo yanayowezekana!


Viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wanapongeza hatua iliyokwishafikiwa kati ya Serikali ya Marekani na Cuba ya kutaka kurudisha mahusiano ya kidiplomasia baada ya nchi hizi mbili kupimana nguvu kwa kipindi cha zaidi ya miaka hamsini. Mkutano wa VII wa Wakuu wa Nchi za Bara la Amerika uliokuwa unafanyika nchini Panama kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 11 Aprili, 2015 umekuwa ni fursa ya kuweza kuwakutanisha viongozi wakuu wa Serikali ya Cuba na Marekani; tukio ambalo kwa wengi limefungua ukurasa wa matumaini.

Rais Barack Obama wa Marekani katika hotuba yake amebainisha kwamba, vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba vimepitwa na wakati na kwamba, anatarajia kuwasilisha wazo hili kwenye Congress ya Marekani, ili viweze kufutwa na hatimaye, kurejesha mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. Viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wanasema, hii ni hatua kubwa na wanatambua kinzani na vikwazo vilivyopo, lakini kukiwepo na utashi wa kisiasa, vikwazo hivi vinaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na wananchi wa pande hizi mbili wakaendelea kushirikiana kwa dhati.

Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema kwamba, hizi ni dalili njema za Jumuiya ya Kimataifa kuanza kujikita katika hija ya amani licha ya kinzani na chuki zilizodumu kwa kipindi kirefu; kwa hakika, amani na upatanisho ni jambo ambalo daima linawezekana ikiwa kama watu wataonesha utashi wa kisiasa na kimaadili. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kuhamasisha majadiliano na maelewano ya dhati baina ya pande hizi mbili. Ni matumaini ya viongozi wa Kanisa kwamba, Cuba itaondolewa kwenye orodha ya nchi ambazo zinafadhili ugaidi duniani sanjari na kusitisha vikwazo vya uchumi ambavyo vimesababisha mateso makali kwa wananchi wengi wa Cuba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.