2015-04-13 11:10:00

Msiogope kusoma alama za nyakati na kupyaisha karama za mashirika yenu


Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani watawa wanaalikwa kwa namna ya pekee na Mama Kanisa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Kutokana na changamoto zinazoendelea kuwakabili watawa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe wa matashi mema, washiriki wa kongamano la juma 44 la kitaifa la watawa lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salamanca, Hispania, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Kumbu kumbu, leo na kesho: maisha ya kitawa miongoni mwa Watu wa Mungu.

Maadhimisho ya mwaka huu yamepewa kipaumbele cha pekee kwani yanakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko unaoendelea kutimua vumbi sehemu mbali mbali za dunia. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anawaombea neema tele kwa kujikita katika karama za waanzilishi wa mashirika yao ya kitawa na kazi za kitume; wawe na ujasiri wa kuzimwilisha karama hizi katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kuwa tayari kuzipyaisha bila woga kwa kusoma alama za nyakati, ili ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu ulielekezwa kwa Padre Carlos Martinez Oliveras. Kongamano hili limefanyika Jimbo kuu la Madrid, Hispania kuanzaia tarehe 9 hadi tarehe 12 Aprili 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.