2015-04-13 10:39:00

Mapambano dhidi ya umaskini ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya


Kardinali Oscar Andrès Rogriguez  Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anabainisha kwamba, Kanisa litaendelea kujifunga kibwebwe ili kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni dhamana inayotekelezwa na Mama Kanisa katika masuala ya kijamii kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Dhamana hii inafumbatwa katika Injili na kufafanuliwa kwa kina na mapana katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kusaidia mchakato wa Jumuiya ya kimataifa kujikita katika misingi ya maadili na utu wema, kwa kuelekeza sera na mikakati ya uchumi ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi badala ya mwelekeo wa sasa wa kutafuta faida kubwa kwa mateso na mahangaiko ya binadamu, yaliyopelekea myumbo wa uchumi kimataifa.

Kardinali Maradiaga ameyasema haya hivi karibuni wakati alipokuwa anachangia mada kwenye kongamano la kitaifa la masuala ya kiuchumi huko Fafe, nchini Hispania. Anasema, neno nidhamu linaonekana kuwa ni kero sana kwa wanachi wengi Barani Ulaya, kwani limekuwa likitumiwa na wanasiasa pamoja na wachumi kuwataka wananchi wa Ulaya kujifunga mikanda ili kubana matumizi katika fedha ya umma. Lakini ikumbukwe kwamba, nidhamu ni fadhila ambayo Kanisa linapenda kuikazia katika maisha na utume wa Familia ya Mungu.

Ni kweli kwamba, sera na mikakati iliyobainishwa na Shirika la Fedha Kimataifa, IMF, bado haijaonesha matokeo yanayokusudiwa katika mchakato wa maboresho ya uchumi na matokeo yake watu wengi wanazidi kupoteza fursa za ajira na hali ya maisha kuwa ngumu, kuliko ilivyokuwa kwa siku za nyuma. Hata leo hii kuna kundi kubwa la watu ambalo limesahauliwa katika mchakato wa sera za uchumi kimataifa, kutokana na ubinafsi, uchu wa mali na kutafuta faida kubwa, mambo yanayoshindwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu.

Kardinali Maradiaga anabainisha kwamba, mchakato wa Uinjilishaji mpya unagusa mahitaji mtu mzima: kiroho na kimwili, kumbe, mapambano dhidi ya baa la ujinga, umaskini na magonjwa ni sehemu ya Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.  

Kuna kundi kubwa la watu wanaotamani kuona na kuonja haki jamii ikimwilishwa katika uhalisia wa maisha. Lengo ni kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata maisha bora kwa kuwa na mgawanyo bora zaidi wa rasilimali na utajiri wa dunia. Itakumbukwa kwamba, upendeleo kwa maskini unaotekelezwa na Mama Kanisa ni dhana inayofumbatwa katika maisha na utume wake kuliko hata mwono wa kijamii, kifalsafa na kisiasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.