2015-04-13 14:47:00

Komesheni nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake na watoto!


Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono juhudi na mikakati ya makusudi inayofanywa na Jumuiya ya Kimataifa ili kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu ambazo wakati huu zinawekwa rehani. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, nyanyaso na dhulumu kwa wanawake na watoto zinakomeshwa na hatimaye, haki msingi zinatawala na kushamiri katika maisha ya watu, ili kujenga amani, utulivu na upendo. Inasikitisha kuona kwamba, wanawake na watoto wananyanyasika sana kwenye maeneo ambayo kuna vita na kinzani za kijamii na kisiasa.

Haya yamebainishwa hivi karibuni na Maria Cristina Perceval, Mwakilishi wa kudumu wa Argentina kwenye Umoja wa Mataifa aliyekuwa ameambatana na Bibi Leila Zerrougui kutoka Algeria, Bi Zainabu Bangura kutoka Sierra Leone pamoja na Julienne Lusenge kutoka Jamhuri ya Watu wa Congo. Viongozi ambao wanawakilisha Jumuiya ya Kimataifa.

Wakati wa mazungumzo yao, wanasema kwamba, wameshirikishana na Baba Mtakatifu Francisko umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria na demokrasia; upatanisho na maridhiano ya kijamii; haki na amani. Ni changamoto ya kuzuia vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, watu wanaopatikana na hatia ya kunyanyasa na kudhulumu wanawake na watoto wafikishwe mbele ya mkondo wa sheria, ili haki iweze kutendeka.

Bibi Perceval anasikitika kusema kwamba, mara nyingi wahusika wa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto hawachukuliwi hatua zinazostahili, ili kutoa fundisho kwa watu wanaodhalilisha utu na heshima ya wanawake na watoto. Wanawake na watoto ni waathirika wakubwa wa vita, kinzani na misigano ya kidini, kisiasa na kikabila, kumbe kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa haki na amani, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa kuwaingiza tena waathirika wa vitendo vya unyanyasi na madhulumu katika familia na jamii husika badala ya kuwatelekeza na hivyo kuwasababishia madonda zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.