2015-04-12 09:25:00

Madonda matakatifu ya Yesu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 12 Aprili 2015 amemtangaza Mtakatifu Gregori wa Narek kuwa Mwalim wa Kanisa. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anasema kwamba, amani ni zawadi ya kwanza ambayo Yesu Kristo mfufuka aliwapatia wafuasi wake waliokuwa bado wamekandamizwa na woga. Alipowaonesha madonda yake matakatifu, wakajazwa na furaha kuu. Hata baada ya siku nane, Mtakatifu Toma ambaye hakuwepo siku ile ya kwanza ya Juma, alioneshwa pia madonda matakatifu, ili aweze kuwa kweli ni shuhuda wa ufufuko wa Kristo.

Mtakatifu Yohane Paulo II alitangaza Jumapili ya pili ya kipindi cha Pasaka kuwa ni Jumapili ya huruma ya Mungu, Yesu kwa njia ya Injili anaonesha madonda yake matakatifu, madonda ya huruma, mwaliko wa kumwangalia na kumgusa kama alivyofanya Mtakatifu Toma, ili wapate kumwamini na hatimaye, kuzama katika Fumbo la upendo wenye huruma uliojionesha kwa namna ya pekee kwa: kwa wadogo na wanyonge. Ni kielelezo cha damu ya Mwanakondoo wa Mungu inayoendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia. Damu hii inaweza kuonekana kwa njia ya madonda matakatifu, ili pamoja na Bikira Maria, Kanisa linaweza kusema, huruma yake hudumu kwa vizazi hata vizazi.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, hata leo hii licha ya majanga mbali mbali yanayomwandama mwanadamu, kutokana na kukosekana kwa upendo, wema na maisha, ni Mwenyezi Mungu peke yake anaweza kumkirimia mwanadamu wema na huruma yake, kwa kufungua mioyo na historia ya maisha ya binadamu. Yesu Kristo aliyefanyika mwili, akazaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, anamkrimia mwanadamu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Ni changamoto ya kutoka katika utumwa wa dhambi na kuingia katika maisha na amani kwa kufuata njia ya madonda matakatifu ya Yesu Mfufuka.

Baba Mtakatifu Francisko anasema waamini wanafundishwa kwamba,  dunia inaweza kubadilika na kuwa ni mahali pema zaidi pa kuishi ikiwa kama watu watajikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu. Kwa kuyaangalia madonda matakatifu ya Yesu, waamini wanaweza kuimba pamoja na Kanisa upendo na huruma yake vyadumu milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.