2015-04-12 11:16:00

Kwa njia ya mifano na ushuhuda wa maisha yenu, waonesheni vijana utawa


Walezi kutoka katika mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume, wamehitimisha kongamano la malezi kimataifa lililokuwa linafanyika mjini Roma kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Kardinali Braz deĀ  Avis, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume katika Ibada ya misa takatifu kwa ajili ya kufunga rasmi kongamano la malezi kimataifa, Jumamosi, tarehe 11 Aprili 2015 amewataka walezi kuhakikisha kwamba, wanawasaidia vijana kumfahamu na kumpenda, ili hatimaye, waweze kumtumikia Yesu Kristo kwa kujisadaka katika maisha ya kitawa.

Kardinali De Aviz amewataka walezi kuwasaidia vijana wao kuishi kadiri ya Injili ya Kristo, dhamana ambayo wamekabidhiwa na Kanisa kwa njia ya mashirika yao. Walezi nao watambue kwamba, wanahamasishwa na kuchangamotishwa na Mama Kanisa kujikita katika hija ya kumfuasa pamoja na kuendelea kumjifunza Kristo, Bwana na Mwalimu. Watambue kwamba, Yesu Mfufuka, yuko hai na anaendelea kutembea pamoja nao katika hija ya majiundo makini na kamwe wasiwe ni watu wenye shingo ngumu kuamini na kumshuhudia Kristo kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko.

Walezi waendelee kujifunza safari za Mababu wa imani katika maisha na miito yao, kama walivyofanya Ibrahim Baba wa imani na Musa, lakini zaidi watawa wamjifunze Yesu Kristo, kwa kuwa waaminifu na wadumifu katika maisha na wito wao, ili kuonja upendo utakaowasaidia kuwafariji wale wanaoteseka. Watawa wajifunze kuwa na imani thabiti kama iliyooneshwa na Mtakatifu Petro na Yohane, wakawa tayari kucharazwa viboko hadharani, lakini wakatangaza na kushudia imani kwa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka wafu.

Wawezeshaji mbali mbali wamewataka watawa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wakiwa huru pasi na kumezwa na malimwengu; wakisimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu pamoja na kuwafichua wale wote wanaoendelea kumdhalilisha mwanadamu kwa kumtumbukiza katika utumwa mamboleo. Ikumbukwe kwamba, watawa wanapaswa pia kufundwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano ndani ya jamii.

Walezi kwa njia ya mifano ya maisha yao adili, washuhudie mashauri ya kiinjili katika malezi yanayomkumbatia mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kutambua kwamba, leo hii, kuna tunu ambazo kama hazijafundishwa vyema na kushuhudiwa kikamilifu, zinaweza kuonekana kana kwamba, zimepitwa na wakati: Haya ndiyo mashauri ya kiinjili yaani: Utii, ufukara na useja. Walezi watambue changamoto na kinzani zilizopo ili kweli waweze kuwasaidia vijana wanaotaka kujisadaka kwa njia ya maisha ya kitawa na kazi za kitume kuweza kuuishi wito wao barabara.

Upendo leo hii ni fadhila ambayo inagubikwa na majanga mengi, watawa wasipokuwa makini, watajikuta wanaogelea kwenye magonjwa yasiyokuwa na kinga wala tiba; watakanganyikiwa na kupoteza imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake; wataona kwamba, Mwenyezi Mungu aliwadanganya na kuwa wamepoteza dira na njia ya kufuata. Vijana waelimishwe umuhimu wa kujisadaka katika mashauri ya Kiinjili kwa ajili ya huduma makini, sifa na utukufu wa Mungu.

Mashirika ya kitawa na kazi za kitume hayana budi kuhakikisha kwamba, yanawaandaa walezi watakaopewa dhamana ya kuwafunda watawa wa mashirika yao, kwa kubainisha malengo na mbinu mkakati wa kuweza kufikia malengo haya. Malezi ni mchakato endelevu katika maisha ya mtawa unaojikita katika maisha ya kiroho, kiutu na katika mahusiano na watu wengine, ndani na nje ya jumuiya. Walezi wajitahidi kumfahamu mtu mzima: kiroho, kimwili na kisaikolojia, ili waweze kumsaidia kijana anayetaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya maisha ya kitawa.

Walezi wameshirikishana fursa, changamoto na vizingiti vinavyojitokeza katika mchakato wa utamadunisho wa karama za mashirika yao katika Makanisa mahalia; mahusiano na walimwengu hususan nyakati hizi za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wamekazia umuhimu wa kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya vijana kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kama njia ya utekelezaji wa mkakati wa Uinjilishaji mpya.

Watawa watambue kwamba, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo vya majadiliano ya kidini na kiekumene, kumbe, malezi ya awali na endelevu hayana budi kugusia nyanja hizi, ili kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na utume wake kwa ukamilifu zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.