2015-04-12 10:17:00

Fursa, changamoto na matatizo ya Kanisa nchini Kenya kujadiliwa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, linaanza hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 17 Aprili 2015. Hii ni fursa ya kukutana, kusali na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake wakuu mjini Vatican. Ni nafasi ya Maaskofu kutembelea na kusali kwenye Makanisa mbali mbali hapa Roma, hasa wakati huu, Kanisa linapojiandaa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, uliotangazwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 11 Aprili 2015 wakati wa masifu ya kwanza ya Jumapili ya huruma ya Mungu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linafanya hija ya kitume mjini Vatican muda mfupi tu tangu yalipotokea mashambulizi ya kigaidi yaliyosababishwa na Kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab, kutoka Somalia na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa wanafunzi wa Chuo kikuu cha Garissa, nchini Kenya. Hili ni tukio ambalo limeacha madonda ya kudumu, hasira na chuki dhidi ya magaidi. Baba Mtakatifu Francisko alionesha masikitiko yake na kuwataka wananchi wa Kenya kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, kamwe wasikubali kumezwa na misigano na chuki za kidini.

Padre Daniel Rono, Katibu mkuu mtendaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anabainisha kwamba, Kanisa nchini humo kwa sasa linakabiliwa na ukata wa rasilimali fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya Kanisa linaloendelea kukua na kupanuka siku hadi siku, lakini miundo mbinu imebaki ni ile ile iliyoanzishwa na Wamissionari miaka kadhaa iliyopita.

Kanisa linapenda kuwekeza zaidi katika majiundo makini ya Wakleri na Watawa watakaojitosa bila ya kujibakizwa kwa ajili ya kuihudumia Familia ya Mungu ndani na nje ya Kenya. Kanisa limeendelea kuwa ni sauti ya kinabii inayowawakilisha wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linataka kuwekeza maradufu katika mawasiliano ya jamii, ili kuwafikia wananchi wengi nchini Kenya, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Padre Rono anasikitika kusema kwamba, udini, ukabila, umajimbo, rushwa na ufisadi ni mambo ambayo yanaendelea kuwameng’enya na kuwagawa wananchi wa Kenya, kiasi cha kushindwa kujenga umoja, mshikamano na mfungamano wa kitaifa, kwa ajili ya mafao ya wengi. Kanisa linaendelea kutoa sauti ya kinabii, kwa kutaka uwepo mgawanyo bora zaidi wa rasilimali na utajiri wa nchi; kwa kuzingatia utawala wa sheria na demokrasia makini.

Uwepo wa Maaskofu Katoliki Kenya mjini Roma, itakuwa ni furaha na faraja kwa Familia ya Mungu kutoka Kenya inayoishi hapa Roma kuweza kukutana na kuzungumza na viongozi wao, ili kufahamu kwa kina na mapana kile kinachoendelea nchini Kenya. Hii ni fursa ya kusali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kenya katika ujumla wake. Familia ya Mungu nchini Kenya inaalikwa kuwasindikiza Maaskofu katika hija yao ya kitume mjini Vatican, ili waweze kufanikisha malengo ya hija hii kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa AMECEA. 








All the contents on this site are copyrighted ©.