2015-04-11 10:56:00

Waraka wa Maadhimisho ya Jubilee ya Huruma ya Mungu: Sura ya huruma


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Machi 2015 wakati wa maadhimisho ya Ibada ya toba, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alitangaza Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, utakaozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2015, kwa kufungua Mlango Mtakatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Jubilee kuu ya huruma ya Mungu itafungwa tarehe 20 Novemba 2016 wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Kristo Mfalme wa ulimwengu.

Baba Mtakatifu, Jumamosi tarehe 11 Aprili 2015, kwenye Mkesha wa Jumapili ya Huruma ya Mungu ametangaza rasmi Waraka wa Maadhimisho ya Jubilee kuu ya huruma ya Mungu unaojulikana kama “Misericordae vultus” “Sura ya huruma”. Baba Mtakatifu katika waraka huu wa kitume anafafanua malengo ya Mwaka wa huruma ya Mungu na mwongozo unaotakiwa kufuatwa, ili kuhakikisha kwamba, waamini wanauishi mwaka huu kwa ukamilifu zaidi.

Waraka huu umegawanyika katika sehemu kuu tatu: sehemu ya kwanza baba Mtakatifu anafafanua kwa kina na mapana dhana ya huruma; sehemu ya pili anabainisha mambo msingi yanayopaswa kutekelezwa wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya huruma ya Mungu na sehemu ya tatu inajikita katika mwaliko. Na mwishoni waraka huu unahitimishwa kwa maombi kwa Bikira Maria, shuhuda wa huruma ya Mungu. Katika maadhimisho ya Masifu ya kwanza ya Jumapili ya Huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko amewakabidhi Waraka wa Sura ya Huruma wawakilishi wa Makanisa mahalia, ili waweze kuwafikishia waamini wao huko waliko.

Sehemu ya kwanza: Dhana ya huruma:

Baba Mtakatifu anafafanua maana ya ufunguzi wa lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tukio litakalofanyika hapo tarehe 8 Desemba 2015, wakati wa Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili. Huyu ni Mama ambaye, amepata upendeleo wa hali ya juu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi cha kumkinga na dhambi, akawa mtakatifu na kujazwa wingi wa upendo wa Mungu, ili kutowacha binadamu kuogelea katika lindi la ubaya.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 8 Desemba 2015, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulipohitimishwa na hivyo kuliwezesha Kanisa kuvunja kuta zilizolitenga na hivyo kuonekana kama mji uliokuwa na upendeleo wa pekee na badala yake, likapata nguvu na ujasiri wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kutumia mbinu mpya. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, Kanisa linapaswa kutumia dawa ya huruma ya Mungu badala ya kukumbatia silaha za sheria kali.

Baba Mtakatifu anatangaza kwamba, kunako tarehe 13 Desemba 2015, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano litafungulia na kwa mtindo huo huo, Makanisa makuu ya Kipapa yaliyoko mjini Roma yatafungua malango yake. Makanisa mahalia pamoja na madhabahu sehemu mbali mbali za dunia, yatapaswa pia kufungua malango ya huruma ya Mungu, ili kuwawezesha waamini kuadhimisha Jubilee ya huruma ya Mungu katika majimbo yao. Hiki ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa zima.

Huruma ya Mungu ni nguzo kuu ya Kanisa:

Huruma ya Mungu ni njia inayomuunganisha Mungu na mwanadamu kwani inafungua moyo wa mtu katika matumaini kwa kutambua kwamba, daima anapendwa, licha ya mapungufu na udhaifu wake wa kibinadamu. Huruma ya Mungu ni sheria makini inayojikita katika moyo wa mwanadamu na nguzo inayolisimamisha Kanisa. Hiki ni kielelezo makini cha maisha ya imani ya Kanisa. Hapa Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa nguvu ya Mungu. Anakiri kwamba, huruma ya Mungu ni ya milele na kwamba, mwanadamu daima ataendelea kuwa chini ya jicho la huruma ya Mwenyezi Mungu. Yesu katika maisha na utume wake, anafafanua maana ya huruma kwani Yeye ni chemchemi ya kielelezo cha upendo unaotolewa kama sadaka.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, upendo ni kielelezo cha utendaji wa Mungu Baba na unakuwa ni kielelezo cha kuwatambua watoto wake wa kweli. Kimsingi, Wakristo wote wanachangamotishwa kumwilisha huruma, kwani wao wamekuwa ni watu wa kwanza kuonja huruma; kwa kupata msamaha wa dhambi zilizotendwa, kumbe, ni jambo la msingi kwa Wakristo kutambua fursa hii. Mara nyingi watu wanadhani kwamba, si rahisi kuweza kusamehe, lakini ikumbukwe kwamba, msamaha ni chombo ambacho kimewekwa mikononi mwa binadamu wadhaifu, ili kuweza kupata utulivu moyoni, ili hatimaye, kuishi kwa furaha.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, imani kwa Kanisa inajikita katika njia ya upendo wenye huruma na unaoguswa na mahangaiko ya wengine. Pengine, kwa miaka mingi, Kanisa halikutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato unaopania kumwilisha huruma, kwa kutumbukia katika kishawishi cha haki, lakini ukweli wa mambo mintarafu utamaduni mamboleo msamaha wa kweli ni changamoto kubwa kutokana na ugumu wa mioyo ya watu. Hapa Mama Kanisa anatumwa kuwatangazia watu furaha ya huruma ya Mungu inayochipua maisha mapya na kuwakirimia watu matumaini ya kuangalia yale yajayo kwa matumaini.

Kauli mbiu ya Jubilee: “Iweni wenye huruma kama alivyo Baba Yenu wa Mbinguni”

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, dhana ya huruma ya Mungu ni sehemu ya maisha na utume wake kama inavyojionesha hata katika Nembo yake ya Kiaskofu “Miserando atque eligendo” maneno ambayo wakati wote yameendelea kumshangaza katika maisha yake. Baba Mtakatifu anafafanua umuhimu wa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu katika ulimwengu mamboleo, kwa kuonesha ari na mwamko sanjari na mikakati mipya ya shughuli za kichungaji, kwani haya ni mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, ili liweze kuaminika katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Mahali ambapo kuna Kanisa, hapo huruma ya Mungu inapaswa kujionesha; mahali penye wakristo, hapo pawe ni chemchemi ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha sehemu ya kwanza ya waraka huu wa kitume Sura ya huruma kwa kufafanua kauli mbiu ya Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu kwa kuwataka waamini kuwa kweli wenye huruma kama alivyo Baba yao wa Mbinguni.

Sehemu ya Pili: Jinsi ya kuishi kikamilifu Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu

Katika sehemu hii, Baba Mtakatifu anaonesha mambo msingi ambayo waamini wanapaswa kuyazingatia ili kweli kuishi kikamilifu maadhimisho ya Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu. Kwanza kabisa anawaalika kufanya hija ya maisha ya kiroho, inayowadai sadaka na majitoleo ya maisha. Anawaalika waamini kutowahukumu au kuwanyooshea wengine kidole, bali wajitahidi kusamehe na kujisadaka.

Hapa waamini wanachangamotishwa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, wanaondokana na mambo ambayo yanasababisha majungu na wivu kwa kupokea mema yanayojikita katika maisha ya jirani zao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya msamaha. Waamini wawe na ujasiri wa kufungua mioyo yao kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha: kwa kufariji na kuonesha huruma; kwa njia ya mshikamano na upendo kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Wakristo wasimame kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu pamoja na kusikiliza kwa makini kilio chao. Wakristo wakiunganika kwa pamoja wanaweza kuvunjilia mbali kuta za utengano na hali ya kutojali wengine; mambo ambayo kimsingi yanaficha ndani mwake unafiki na ubinafsi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutenda matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa kuasha ndani ya dhamiri zao moyo wa kuona mateso na mahangaiko ya watu wanaoteseka kutokana na baa la umaskini. Wakristo wanakumbushwa kwamba, utume wa Yesu hapa duniani ulikuwa ni kuwafariji maskini na kutangaza kufunguliwa kwa wafungwa na hata waathirika wa utumwa mamboleo; kuwapatia watu wanaojitafuta wenyewe, mwelekeo mpya wa maisha; kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, kwa kushinda kishawishi cha ujinga ambacho bado kinaendelea kuwaandama watu wengi katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anaangalisha kuhusu mapadre waliopewa dhamana ya kuondolea dhambi zilizotengwa kwa ajili ya “kiti cha kitume”. Waungamishaji wanapaswa kutambua kwamba, wao ni alama ya huruma ya Mungu, dhamana wanayopaswa kujiandaa kuitekeleza kwa makini, wao wenyewe wakiwa ni watu wa kwanza kuomba toba na maondoleo ya dhambi.

Mapadre wawe ni wahudumu waaminifu wa huruma ya Mungu, kwa kuwapokea waamini wanaokwenda kutubu kama alivyofanya Baba mwenyehuruma, licha ya dhambi na mapungufu ya waamini wao. Waungamishaji wawe ni watu wa huruma bila kuuliza maswali yanayoweza kumkera mwamini, ili kuwapokea waamini wanaomba msaada na huruma ya Mungu. Waungamishaji wawe ni alama ya kwanza kabisa ya huruma ya Mungu kwa waamini wao, wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya kutoa Sakramenti ya Upatanisho.

Katika maadhimisho ya Jubilee ya huruma ya Mungu, Kipindi cha Kwaresima, Baba Mtakatifu atawatuma Mapadre maalum kuwaondolea watu dhambi ambazo zimetengwa kwa ajili ya kiti cha kitume, kama alama ya upendo unaobubujika kutoka kwa Mama Kanisa. Ni wajumbe watakaoonesha utu na ubinadamu; chemchemi ya uhuru kamili; kwa kuwajibika kikamilifu ili kuondokana na vikwazo pamoja na vizingiti mbali mbali, tayari kuanza maisha mapya yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, rehema kamili ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa maadhimisho ya Jubilee, kwani Mwenyezi Mungu daima yuko tayari kusamehe dhambi bila mipaka. Dhambi zinaondolewa kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, lakini kwa njia ya rehema kamili, mwelekeo hasi wa dhambi unaondolewa kutokana na mabaki ya dhambi yanayobaki katika mawazo na matendo ya waamini. Hapa Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, ili kupata rehema kamili wanapaswa kutenda kwa upendo, kukua na kukomaa katika fadhila ya upendo badala ya kuendelea kuanguka dhambini.

Sehemu ya tatu: Mwaliko dhidi ya uhalifu, rushwa na ufisadi

Sehemu hii ya tatu ya Waraka wa Kitume "Uso wa Huruma", Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee makundi ya kihalifu, kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuanza ukurasa mpya wa maisha, unaojikita katika huruma ya Mungu. Fedha si chemchemi ya furaha ya kweli kwani inadanganya na kumpumbaza mtu. Kutumia uhalifu ili kupata fedha inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia, inawadhalilisha na kwamba, hakuna mtu anayeweza kukwepa hasira na hukumu ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka watu wanaotoa na kupokea rushwa kuacha mara moja tabia hii, kwani huu ndio muda uliokubalika wa toba na wongofu wa ndani, kwani rushwa ni saratani mbaya ambayo kilio chake kinamfikia Mwenyezi Mungu mara moja, kwani inaharibu msingi wa maisha na mfungamo wa kijamii na kwamba, fedha haiwezi kamwe kugeuzwa kuwa ni miungu ya watu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuondokana na saratani hii katika maisha ya kijamii. Watu wawe na ujasiri kuondokana na saratani hii katika maisha yao binafsi, kwa kuwa macho, kwa kujikita katika hekima, ukweli na uwazi na kuwa na ujasiri wa kufichua vitendo vya rushwa na ufisadi.

Baba Mtakatifu anakazia mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo, Waislama na Wayahudi kwani katika vitabu vitakatifu vya dini hizi, huruma ya Mungu inapewa kipaumbele cha kwanza. Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilee iwe ni fursa ya kuimarisha majadiliano ya kidini, kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kuondokana na vurugu na vitendo vya ubaguzi.

Baba Mtakatifu anakazia mahusiano kati ya haki na huruma; fadhila zinazolandana na kukamilishana. Yesu aliwaonesha binadamu zawadi kubwa kwa kuwapatia huruma na msamaha wa dhambi na kwamba, haki ya Mungu inajikita katika huruma yake. Huruma ni kiini cha maisha na utume wa Yesu hapa duniani na kwamba, watu wanaokolewa kwa kuwa na imani kwa Yesu Kristo. Kumbe, haki na huruma ni fadhila ambazo Mwenyezi Mungu anazitumia kwa wadhambi ili kutubu, kuongoka na kupata msamaha wa dhambi zao. Lakini Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, mtu anayekosa itampasa adhabu, kama sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu na kwamba, upendo ni msingi thabiti wa haki ya kweli.

Hitimisho:

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Waraka wake wa Kitume: Uso wa huruma kwa kumwangalia Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu, ambaye maisha yake yalipambwa kwa huruma ya Mungu iliyofanyika mwili. Ni sanduku la agano kati ya Mungu na mwanadamu. Bikira Maria anaonesha kwamba, huruma ya Mungu haina mipaka inawafikia wote na hakuna hata mmoja anayeweza kutengwa nayo. Mtakatifu Faustina Kowalska alibahatika kuzama katika huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi ili aweze kuwashangaza, kwani kamwe hachoki kufungua malango ya moyo wake kwa binadamu. Dhamana ya kwanza ya Kanisa ni kuhakikisha kwamba, inawasaidia watu kufahamu Fumbo la huruma ya Mungu, kwa kuutafakari uso wa Yesu, hasa kwa nyakati hizi ambamo kuna matumaini makubwa lakini pia kinzani.

Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu utafungwa rasmi hapo tarehe 20 Novemba 2016, Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, miaka ijayo itapambwa na huruma ya Mungu, ili kuweza kukutana na kila mtu, ili kumwonjesha wema na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waguswe na mafuta ya huruma ya Mungu kama alama ya Ufalme wa Mungu, ambao uko miongoni mwa watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.