2015-04-11 12:27:00

Walezi ni matumaini ya vijana wengi wanaotaka kujisadaka katika utawa


Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza na kuwashukuru watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia walioshiriki katika kongamano la malezi kimataifa kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, uliofunguliwa kwa mkesha wa Sala, tarehe 7 Aprili na kuhitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu tarehe 11 Aprili 2015 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali Braz de Aviz, Rais wa Baraza la Kipapa la mashirika ya kitawa na kazi za kitume.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake anasema, changamoto kubwa kwa watawa wa nyakati hizi ni kuishi ndani ya Kristo mintarafu maisha ya Kiinjili, kauli mbiu ambayo imefanyiwa kazi wakati wa kongamano la kimataifa, lililowashirikisha mabingwa mbali mbali katika malezi na majiundo ya kitawa na kipadre. Walezi wanakumbushwa kwamba, wao ni matumaini ya vijana wengi ambao wanasukumwa na upendo wa Kristo, wanatafuta ndani ya Kanisa nafasi ya kuweza kuumwilisha kwa njia ya huduma kwa Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, idadi ya watawa inaendelea kupungua kwa kasi kubwa sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, kuna haja ya kujikita katika malezi makini yatakayowaandaa vijana mintarafu Moyo Mtakatifu wa Yesu. Pale ambapo watawa wameshuhudia wito na utume wao kwa moyo mkuu na unyenyekevu, huku wakijitahidi kumwilisha karama za mashirika yao katika Makanisa mahalia, hapo kuna miito mingi ambayo imechipuka na kukua kwa wingi.

Walezi wanatakiwa kuwa ni mashuhuda na wafuasi amini wa Yesu Kristo mintarafu karama za mashirika yao. Kila siku ya maisha yao, watawa wajitahidi kuonesha ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Walezi wahakikishe kwamba, wanajitahidi kujilea wao wenyewe kwanza kabla ya kujikita katika malezi ya vijana wanaodhaminishwa kwao na mashirika yao, kwa kujenga na kuimarisha urafiki wa karibu na Yesu Kristo, Mwalimu na Bwana.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, maisha ya kitawa ni kati ya amana kubwa ambazo Mama Kanisa amekirimiwa katika maisha na utume wake hapa duniani, kwani watawa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Mashauri ya Kiinjili wanafuata maisha ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Wakati mwingine, watawa wanaweza kudhani kwamba, wito na maisha yao ni mzigo mzito usioweza kubebeka, lakini hiki ni kishawishi na ulaghai. Watawa watambue kwamba, wito na maisha yao ni amana muhimu sana, changamoto na mwaliko wa kuijunda mintarafu utume na ari ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kila mahali, lakini zaidi kwa kuwaonjesha maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, upendo wa Kristo. Watawa wajiweke mbele ya maskini, ili waweze kuwainjilisha pia, jambo linalohitaji msingi thabiti, ambao kwa bahati mbaya, familia nyingi zinashindwa kuujenga, jambo ambalo linaongeza dhamana na wajibu wa walezi katika maisha ya kitawa na kazi za kitume.

Baba Mtakatifu anawataka walezi kuwa na mapendo makuu kwa vijana wanaowafunda, ili kuwajengea uwezo wa kuwakaribisha na kuwakumbatia wote, wakiwa na wingi wa huruma na mapendo; walezi wawe ni baba na mama, kwa kujitahidi kutoa malezi kadiri ya uwezo wao, jambo linalowezekana ikiwa kama linasukumwa na upendo unaooneshwa na wazazi.

Si kweli kwamba, vijana wa kizazi kipya ni wachoyo na hawawezi kujisadaka kwa ajili ya wengine, lakini wanapaswa kuonja na kutambua kwamba, ni vyema zaidi kutoa kuliko kupokea; kuna uhuru mkubwa katika maisha ya utii, usafi kamili na ufukara. Hapa walezi hawana budi kuhakikisha kwamba, wanakuwa makini katika kila hatua ya malezi kwa vijana, kwa kuwa na mang’amuzi mapana ili kupata watawa bora, wachapakazi na watakatifu. Malezi hayana budi kuwa ni sehemu ya mchakato wa maisha ya mtawa, kwa kuwasaidia vijana kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwafunda barabara, katika: maisha, utume, udugu na tafakari ya kina.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru walezi wa mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume kwa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya kuwafunda vijana, changamoto ni kuendelea kuitekeleza dhamana hii pasi na kujibakiza wala kukatishwa tamaa. Madhaifu na mapangufu yanayoweza kujitokeza yawe ni kikolezo cha majiundo makini na endelevu ya walezi, pale ambapo kazi yao inaonekana kutothaminiwa, watambue kwamba, Yesu anawafuata kwa upendo na kwamba, Kanisa kwa upande wake, linatambua na kuthamini mchango na utume wao. Walezi wahakikishe kwamba, wanaishi utume wao kwa furaha kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa ndugu zao katika Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.