2015-04-11 14:50:00

Katekisimu Mpya ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kanisa Katoliki


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina Yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Wakati tukingali bado shangweni mwa Paska tunapenda kukutakia Heri na Baraka tele kwa Adhimisho la Pasaka ya Bwana. Kristo Bwana aliyeshinda dhambi na mauti, anatualika sisi nasi tufufuke kutoka kwa wafu, tufufuke kutoka katika makaburi yetu ya dhambi, makaburi ya vita, manyanyaso, ubaguzi, uonezi, uvivu na kila uzembe, tuwe hai katika Kristo Yesu, tuyatafute mambo ya juu, aliko yeye mwenyewe.

Baada ya kujihinisha kwa mfungo wa Kwaresma, tujaaliwe neema hiyo ya ufufuko. Lakini tuwe makini na kishawishi cha kurudia katika makaburi yetu kwa kasi na ujasiri Zaidi. Kisha kutoka katika kaburi tulilokuwa nalo katika maisha, usilirudie tena. Kristo Mfufuka na akae mioyoni mwetu, atujaze neema zake, tutoke kifua mbele twende tukatangaze Habari njema na Amani ya Kristo Mfufuka kwa watu wote, hasa ndugu zetu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Leo mpendwa msikilizaji tunakuletea utangulizi wa kipindi cha Hazina yetu. Ndani ya kipindi hiki tutajikumbusha mambo msingi ya Imani yetu Katoliki, kadiri inavyoelezwa na Mama Kanisa katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki.

Lengo letu: tunataka nyakati hizi za uinjilishaji wa kina, sote tujibidishe katika kuifahamu vema Imani yetu. Miyumbo mingi ya kiimani na hata mikanyagano mingi ndani ya Kanisa ni kwa sababu wengi wetu hatujabahatika kufahamu vema misingi ya Imani yetu. Tunashukuru na kupongeza sana jitihada zilizopo katika kuyasoma na kuyajifunza maandiko matakatifu kwa walio wengi.  Hiyo ni moja ya vyanzo vikuu vya mafundisho ya Imani yetu. Chanzo kingine ndicho hiki,  tunachotaka kukiwekea Mkazo wa dhati yaani Katekisimu ya Kanisa Katoliki, ambayo ni Muhutasari wa mafundisho yote ya Imani yetu.

Mafundisho yote, tangu historia ya ukombozi ilipoanza kuundwa, hadi Kristo Bwana alivyowapa Mitume na Wafuasi wake, nao wakarithisha vizazi vilivyofuata; na kwa mwanga wa Roho Mtakatifu yakafafanuliwa nyakati mbalimbali, hadi nyakati zetu kwa njia ya Mtaguzo wa Pili wa Vatikani, yote hayo kwa ufupi tunayakuta katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Tutaimega kidogo kidogo hadi mwisho.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ambayo sisi tutakumbushana katika kipindi cha Hazina yetu, ipo katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza inahusu ungamo la Imani. Ndani ya kipengele hiki, tutayaona mawasiliano katika ya Mungu na mwanadamu. Tutamtazama pia mwanadamu kama kiumbe mwenye uwezo wa kumtafuta, kumjua na kuongea na Mungu muumba wake. Na Zaidi tutayona yafuatayo: Ufunuo wa Kimungu, uenezaji wa mafunuo matakatifu, Maandiko Matakatifu; jibu la mwanadamu kwa Mungu, linalijidhihirisha katika Imani yake.  Tutatazama pia ungamo la Imani ya Kikristo, huku tukivifafanua vipengele kumi na viwili tunavyovitamka katika ungamo letu la Imani, yaani kwa lugha iliyozoeleka, Sala ya Nasadiki au Kanuni ya Imani.

Katika sehemu ya pili ya Hazina yetu, tutatazama juu ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kikristo. Ndanimwe, tutaona juu ya maadhimisho ya Sakramenti yanavyokamilishwa katika liturujia kama kazi ya Utatu Mtakatifu, tutatazama pia fumbuo la Paska katika sakramenti za Kanisa, uadhimishaji wa liturujia ya Kanisa, utofauti wa maahimisho ya kiliturujia na umoja wa fumbo hilo la liturujia. Ni katika kipengele hiki mpendwa msikilizaji, tutazichambua sakramenti zote saba, na tutahitimisha kwa kuona maadhimisho mengine ya kiliturujia kama vile visakramenti, pamoja na maziko ya kikristo.

Katika sehemu ya tatu ya Hazina yetu, tutatazama juu ya Maisha katika Kristo. Ndanimwe tutafafanuliwa juu ya hadhi ya mwanadamu, juu ya jumuiya ya binadamu, na juu ya wokovu wa Mungu. Ni katika kipengele hiki tutaona mambo yahusuyo sheria za kimaadili, neema na kufanywa haki, tutajifunza maana ya Kanisa kama Mama na Mwalimu, na juu ya Amri Kumi za Mungu.

Katika sehemu ya nne na ya mwisho ya Hazina yetu, tutatazama juu ya sala za Kikristo; sala katika agano la kale, na sala katika utimilifu  wa nyakati, sala katika nyakati za Kanisa. Hapa ni muhimu kujua pia aina ya sala na namna ya kusali. Katika kipengele hiki, tutaichambua pia ile sala kuu aliyotufundisha Bwana, yaani Baba yetu, tujue undani wake na uzito wake. Kumbusho kubwa tutakalopata hapa ni kwamba, maisha yetu ya imani lazima yapambwe na roho ya kupenda kusali daima, kwani ni agizo la Bwana mwenyewe aliyesema ‘salini bila kuchoka’.

Mafundisho haya ya imani yetu yatatusaidia vema kuitafakari na kuithamini huruma ya Mungu inayokuja kwetu kwa njia mbalimbali. Na sisi tunaalikwa kuiitikia huruma hiyo ya Mungu, kwa kuiishi vema imani yetu, kuwa mashuhuda wa kweli wa uwepo na kazi ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku.

Basi mpendwa msikilizaji tunakualika tusafiri pamoja katika safari ndefu na nzuri ya kuijua/kukumbushwa/kufafanuliwa/kuelekezwa juu ya mafundisho ya imani yetu ya kweli - Katoliki. Hima hima, kaza buti - bila kukata kamba, kaza mwendo wa Imani - twende pamoja tuijue vizuri imani yetu na tukaiishi. Asante kwa kusikiliza Radio Vatican. Ungana nami tena kipindi kijacho wakati kama huu.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Katekista wako - Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.