2015-04-11 17:22:00

Jumapili ya huruma ya Mungu! Toba na wongofu wa ndani!


Jumapili ya leo Kanisa latuagiza kusherehekea Jumapili ya huruma ya Mungu - kutangaza kwa uwazi huruma ya Mungu ikikumbuka magumu na majaribu yaliyo mbele ya mwanadamu. Matayarisho katika kungoja Jumapili hii huanza kwa Novena siku ya Ijumaa Kuu ambayo huhitimishwa Jumapili hii ya leo, Jumapili ya pili ya Pasaka kila mwaka. Sikukuu hii ilitangazwa rasmi hapo Mei 2000 kwa agizo la Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II.

Ibada kwa huruma takatifu ya Mungu ni sehemu ya maisha ya kiroho ya Kanisa. Ibada ambayo Mtakatifu Faustina Kowalska aliyetangazwa mtakatifu tarehe 30/04/2000 aliishi kwa uwazi katika maisha yake na kwa makusudi mazima Baba Mtakatifu aliweka sikukuu hii kutukumbusha huruma ya Mungu inayotawala katika maisha ya kanisa na ulimwengu.

Maisha yake

 

 

Kwamba alizaliwa - angalia Mt. 1:1-17 na Lk. 3:23-38 - ukoo wa Yesu. Aliishi kati ya watu – Lk. 1:39 - Maria anamtembelea Elizabeth 4:14... Yesu anaanza kuhubiri katika Galilaya kwa hiyo alifanya hivyo kati ya watu.  Kwamba alikuwa na wafuasi na mitume ambao walifahamika na watu na majina yao tunayo hadi leo - wito wa mitume -12. Lk. 6:12-16.

Kwamba alifanya miujiza - ufufuo wa Lazaro – Yoh. 11. Kwamba aliteswa - angalia mazingira ya hukumu yake - watu wangapi walihusishwa - Pilato, Herode, Kayafa, Anasi, kuachiliwa kwa Baraka na kadhalika - ni watu ambao waliishi na walishiriki katika siasa ya wakati ule. Historia ya kweli. Hata hapo juu nimesema kuwa kuhusu kuwa Yesu alifufuka fufukaje ni maelezo magumu ila matokeo ya ufufuko wake yameonekana na wengi - hakika ni vigumu kuamini kuwa hayo waliyoshuhudia wafuasi wake ni uwongo mtupu.

Zaidi sana tunasoma katika somo la leo – Yoh. 20:29 - wengine watamsadiki Yesu bila kumwona kwa ushududa wa mitume tu 17:20, Mdo. 1:8. Maisha ya Mt. Faustina ni ushuhuda wa karibu mno kuthibitisha hilo. Orodha ingeweza kuwa ndefu kuthibitisha hilo. Kwa kifupi, maandiko matakatifu ni ushuhuda wa uwepo wa upendo wa Mungu kwetu sisi upendo uliothibitishwa na uwepo wa Kristo kati yetu.

Katika somo la Injili siku ya leo, twaona kuwa maelezo juu ya ufufuko au alifufuka fufukaje yana ugumu wake ila matokeo ya huo ufufuko yanaonekana wazi kwa mfano tunaona katika maandiko matakatifu kuwa kwa kifo na ufufuko wake watu wamepata imani - ufufuko wa Kristo ni sababu ya imani yao.

Mwinjili Marko - Mk. 15:39 - tendo la ufufuko wa Yesu ndiyo sababu ya imani ya yule akida basi yule akida aliyesimama hapo alimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii akasema hakika mtu huyu alikuwa mwana wa Mungu. Kifo chake Yesu ni sababu ya imani yetu – hafi, ila anashinda mauti. Naye Mwinjli Matayo - anaona ufufuko katika kifo cha Yesu - Mt. 27:52-53 - makaburi yakafanuka, ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala, nao wakiisha kutoka makaburini mwao baada ya kufufuka kwake wakauingia mji mtakatifu wakawatokea wengi.

Tena Mwinjili Yohane 19:30 - analinganisha kufa kwa Kristo na kutupatia roho - basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki alisema imekwisha, akainua kichwa akaisalimu roho yake.

Ndugu mpendwa tendo la ufufuko wa Yesu siyo tendo la ushujaa, yaani Yesu anataka kutuonesha kuwa ana uwezo wa kufanya tu tendo la pekee na la kishujaa bali ni ufunguo kwetu kwa neema ya ajabu ya Mungu - hata leo nguvu yake yaonekana katika maisha ya kanisa na mioyo ya waamini. Ndicho kinachonekana katika masomo yetu ya leo; ishara zikafanyika, ushuuda wa Yohane, watu wanaamini katika hilo.

Somo hili la injili - latuingiza katika roho ya siri ya ufufuko. Yesu anawatokea katika chumba cha juu - salamu yake ni amani. Ni salamu iliyojaa neema ya uhakika wa upendo wa Kristo na kwa kila mmoja. Yeye aweza kutoa hiyo amani kwa vile anayo na zaidi sana sasa kwa utukufu kaunganika na Baba atoaye mema yote. Uumbe wake – waondoleeni watu dhambi. Ni sala na utume.

Halafu anawapeleka/anawatuma mitume kama alivyopelekwa yeye mwenyewe. Naye ni mtume wa Mungu – Ebr. 3:1 - kwa hiyo ndugu watakatifu wenye kuushiriki mwito wa mbinguni mtafakarini sana mtume na kuhani mkuu wa maungano yetu yesu aliyetumwa kwa ulimwengu. Ufufuko wahitimisha utume wake sasa. Naye aweza kuwapekeka mitume wake, wale aliowachagua yeye ili wapate kuendeleza kazi hiyo ya upendo wa Mungu kwetu.

Pia karibu kabisa na siri hii ya wokovu ni maneno ya Yesu - pokeeni roho mtakatifu. Katika salamu zake za kuwaaga mitume aliwaambia ni lazima nirudi kwa Baba ili awapelekee roho mtakatifu wa Mungu juu yao – Yoh. – 16:7 lakini mimi nawaambia iliyo kweli yawafaa ninyi mimi niondoke kwa maana mimi nisipoondoka huyo msaidizi hatakuja kwenu bali mimi nikienda zangu nitampeleka kwenu.

Katika hotuba yake siku ya Pentekoste, Mtakatifu Petro anaonesha wazi kuufahamu mpango huu wa Mungu. Anaunganisha vizuri kabisa ufufuko wa Bwana na kupeleka roho mtakatifu. Anasema akiwa ametukuzwa na Baba, Yesu alipokea roho aliyeahidiwa kutoka kwa Baba halafu akamtuma roho huyo kwetu – Mdo. 2:33 - basi yeye akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu na kupokea kwa Baba ile ahadi ya roho mtakatifu amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia. Kupokea kwake roho ni uhakika kuwa naye atupatia roho wa Mungu.

Maandiko yanatuambia kuwa kwa ajili ya utume wake yeye alipokea tayari roho siku ya ubatizo wake – Lk. 3:21-22 - ikawa watu wote waliokwisha kubatizwa na Yesu naye amebatizwa anaomba, mbingu zilifunuka, roho mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili kama hua, sauti ikatoka mbinguni wewe ndiwe mwanangu mpendwa watu nimependezwa nawe.

Hakika ni mapenzi yake baba kuwa ametupatia ukombozi kwa njia hii kwetu ni fumbo kuu la upendo. Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanatupenda upeo kiasi cha kujitoa kwetu. Somo la pili laonesha hilo. Fumbo hili la upendo ni kwa ajili yetu sisi wanadamu. Ufufuko wa Kristo ni ufunguo wa mlango unaoruhusu ujio huu wa neema na upendo wa Mungu kwetu. Kama tukikubali maisha yake ina maana pia twakubali upendo wake ndiyo maana ya ufufuko kwetu.

Hii ndio maana ya Paskaka. Mungu anamweka Yesu awe hakimu wa ulimwengu wazima na wafu. Ametukuzwa juu mbinguni na kazi ya kuwakomboa watu inaendelea ndiyo sababu tuko hapa - hilo tukio lingeishia pale msalabani au kaburini hakika tusingekuwa tunafanya kumbukumbu hii au sherehe hii leo hii. Hivyo ni lazima tuendelee jambo hilo. Mt. Petro anasema kila aaminiye anao msamaha wa dhambi na uzima wa milele - tukiamini na kuishi hivyo tutaokoka.

Katika 1Pt. 1:3 - matumaini yanatuhimiza kuwa watakatifu - kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zetu na kuwa na kiasi, mkiitumaini kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Na katika kuendelea kuishuhudia imani hiyo kati ya wengine - 1Pt. 2:11-12 - tunaona hivi - wapenzi nawasihi, kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho, mwe na mwenendo mzuri kati ya mataifa ili iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya wayatazamapo matendo yenu mazuri wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.

Ndugu yangu mpendwa napenda kukushirikisha mfano huu nikiamini kuwa utasaidia kufanya bidii katika kuyafahamu mapenzi ya Mungu kwetu ili tuweze kushuhudia kikamilifu kama mitume. Ufahamu ni wokovu. Mchungaji mmoja alifika mjini akitaka kwenda ofisi ya posta ili kutuma barua. Kwa bahati mbaya hakuijua vizuri barabara ya kufika mahali hapo. Na pia hakuwa na unyenyekevu  kuuliza wenyeji. Kwa muda mrefu kijana mmoja alimwona akiwa anazungukazunguka katika eneo hilo.

Baada ya muda mrefu akamsogelea na kumwuliza yule mchungaji kama alikuwa anatafuta kitu Fulani. Yule mchungaji akamjibu, nataka kufika ofisi ya posta. Naye kijana bila kusita akageuka na kumwambia mzee ofisi ya posta ile pale mbele ya macho yako. Baada ya kumaliza shuhguli zake pale ofisini, yule mchungaji akatoka, akamshukuru yule kijana lakini pia akamwalika yule kijana kuwa jioni ya siku ile aje kwenye mahubiri yake mazuri atakayotoa juu ya jinsi ya kufika  mbinguni. . Yule kijana alimshukuru lakini akamwambia samahani sitafika. Yule mchungaji akasikitika na kutaka kujua maana ya jibu la yule kijana kukataa mwaliko mzuri namna hiyo. Naye kijana akamjibu akisema, itakuwaje wewe hujui njia ya kufika ofisi ya posta iliyo mbele ya macho yako,  unifundishe mimi kufika mbinguni usikokuona?

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.