2015-04-10 10:37:00

Wafundeni watawa kadiri ya mwanga wa Injili ya Kristo!


Kuna haja kwa mashirika ya kitawa na kazi za kitume kuwa na mbinu mkakati wa malezi ya awali na endelevu, ili kuweza kuwafunda watawa kuwa kweli ni wanyenyekevu na wawajibikaji. Watawa wawe na uwezo wa kujenga na kujipyaisha katika maisha yao kuzunguka Fumbo la Pasaka pamoja na kukumbatia Fumbo la Msalaba, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, mwaliko kwa watawa kumkimbilia Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Hii ni changamoto ambayo inatolewa na Sr. Claudia Pena y Lillo kutoka Santiago wakati alipokuwa anashiriki katika kongamano la malezi kimataifa, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanasoma maisha yao kwa miwani ya hekima, huku wakijitahidi kufundwa na mang’amuzi ya maisha ya kila siku, ili kukua na kukomaa kiroho na kiutu. Waendelee kumjifunza Yesu aliyekuwa ni mwalimu na mlezi makini; aliyefundisha kwa njia ya mifano yake ya maisha, akawaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu; akaponya magonjwa, akaganga njaa na kuwaondolea watu dhambi zao.

Yesu alikuwa na mwono chanya kuhusu maisha ya binadamu, akaonesha kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Watawa wakumbuke kwamba, kama sehemu ya majiundo makini wanapaswa kufundwa na maskini wanaowahudumia. Hii ni changamoto ya kufuata mfano wa ukomavu wa Mtakatifu Petro katika maisha na ufuasi wake, kiasi hata akawa tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Petro alikuwa jasiri katika imani na maamuzi yake, lakini wakati mwingine alionesha udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, lakini akawa tayari kujifunza kutoka kwa Yesu, aliyemwonesha upendo na huruma. Yesu alijkitahidi kujenga utamaduni wa majadiliano na wanafunzi wake, akawasikiliza na kuwafafanulia yale yaliyowatatiza katika hija ya maisha yao. Huu ni mwaliko wa kuyatafakari maisha mintarafu miwani ya imani na neema.

Hivi ndivyo anavyobainisha  Padre Riccardo Volo, Jaalim toka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano. Anawaalika watawa kwenda Galilaya, tayari kutangaza Habari Njema ya Wokovu, mwaliko na changamoto hata kwa walezi wa nyakati hizi. Ni mwaliko wa kufanya hija na kusaidiana na wengine; kwa kusahihishana, kutiana moyo na kufundisha tunu msingi za maisha. Jambo la msingi ni kuwafunda watawa kuwa kweli ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha yao ya kila siku.

Walezi baada ya kusikiliza kwa makini mafundisho ya wahamasishaji wakuu, jioni wanaingia katika makundi, ili kushirikishana mang’amuzi katika safari ya kuwafunda watawa kadiri ya moyo wa Kanisa na ulimwengu. Ni changamoto inayotolewa na Sr. Nicla Spezzati, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Kati ya mada zinazofanyiwa kazi ni vijana wanaoomba kujiunga na maisha ya kitawa; malezi katika nyanja za mawasiliano na mitandao ya kijamii; maskini kama wadau wakuu wa malezi; kukamilishana na kutegemezana kati ya watawa wa kike na kiume katika maisha ya kuwekwa wakfu.

Tema nyingine ni majadiliano na utamadunisho katika malezi. Mambo yote haya yameangaliwa kwa umakini mkubwa, ili kuibua mbinu mkakati unaoweza kutumiwa na watawa kwa siku za usoni. Watawa wajitahidi kuchota matumaini yao kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ili kweli waweze kuwa ni chemchemi ya furaha. Baba Mtakatifu anasema kwamba, mahali walipo watawa hapo kuna furaha, kwani hawa ni watu wanaotambua uwepo wa Kristo Mfufuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.