2015-04-10 14:55:00

Viongozi wana dhamana ya kuwalinda na kuwatetea maskini


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 10 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Giorgi Margavelashvili wa Georgia na baadaye amekutana pia na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Mazungumzo kati ya viongozi hawa wawili katika hali ya upendo, yamewawezesha kujadili kwa kina na mapana mahusiano ya pande hizi mbili sanjari na kupongeza mchango unaotolewa na Kanisa mahalia katika sekta ya elimu, ustawi na maendeleo ya jamii. Viongozi hawa pia wameonesha masikitiko yao makubwa kutokana na kinzani zinazoendelea kujitokeza katika ukanda wa Georgia.

Kwa pamoja wanahimiza umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea sheria za kimataifa na kwamba, suluhu ya amani inaweza kupatikana kwa njia ya majadiliano kwa makundi yanayohusika. Baba Mtakatifu na mgeni wake wamepongeza mchango wa nchi ya Georgia katika maendeleo ya Bara la Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko amemzawadia Rais medali ya Mtakatifu Martino anayemlinda maskini kwa kutumia joho lake kwa kusema kwamba, viongozi na wakuu wa nchi wanayo dhamana ya kuwalinda na kuwatetea maskini na wanyonge bila kuwasahau watu wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.