2015-04-10 09:15:00

Utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi asubuhi tarehe 9 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Andrej Kiska wa Slovakia na baadaye Rais na ujumbe wake wamekutana na kuzungumza pia na Monsinyo Antoine Camillieri, Katibu mkuu Msaidizi wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Viongozi hawa katika mazungumzo yao wamepembua kwa kina na mapana mahusiano ya nchi hizi mbili katika kipindi cha miaka 25 na Jamhuri ya wananchi wa Czech na Slovakia kwa wakati huo; tukio ambalo lilifanyika kunako tarehe 19 Aprili 1990. Baadaye Papa Yohane Paulo II akafanya hija ya kitume nchini humo. Katika kipindi chote hiki kumekuwepo na mafanikio pamoja na mahusiano mazuri kati ya pande hizi mbili. Wamesifu mchakato wa majadiliano kati ya Kanisa na viongozi wa Serikali, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu na mgeni wake, baadaye katika mazungumzo yao wamegusia masuala ya kimataifa, lakini kwa namna ya pekee changamoto zinazoendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo duniani kama vile Mashariki ya kati na kwamba, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.