2015-04-10 09:52:00

Patriaki Bartolomeo wa kwanza: Maisha, utu na heshima ya binadmu!


Kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia kinaendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia, lakini ikumbukwe kwamba, watu wanaweza kushinda ubaya kwa kutenda mema, kwani huu ndio ujumbe makini unaotangazwa na Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka wafu. Huu ni ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka ya Kanisa la Kiorthodox inayoadhimishwa, tarehe 12 Aprili 2015.

Kwa maadhimisho ya Pasaka, Kanisa lina adhimisha kifo cha kifo, chemchemi ya maisha mapya na matumaini; yanayoonesha ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti. Hakuna mtu anayeweza kufuta tofauti iliyopo kati ya watu kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia, hiki ni kielelezo cha udhaifu wao mkubwa katika matendo yanayojikita kwenye mauaji.  Matatizo ya binadamu hayawezi kutatuliwa kwa njia ya mauaji, dhuluma na nyanyaso za kidini, dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anabainisha kwamba, matatizo yanayomwandama mwanadamu yanaweza kupatiwa ufumbuzi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha, utu na heshima ya binadamu; pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea haki zake msingi. Kwa njia ya mateso, kifo ba ufufuko, Yesu ameonesha ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Kanisa linaamini na kutangaza kwamba, maisha ya binadamu ni haki msingi ya kila mtu inayopaswa kulindwa na kudumishwa na wengi.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema kwamba, imani kwa Yesu Kristo Mfufuka ni matumaini kwa binadamu wote, kwani Yeye ni chemchemi ya maisha mapya na wokovu kwa wote. Ni kielelezo makini na mfano wa kuigwa katika kupambana na changamoto za maisha bila ya kukata wala kukatishwa tamaa. Kwa njia ya Yesu, binadamu anaweza kupata utambulisho wake na kumwilisha ujumbe wa ufufuko kwa imani na matumaini.

Yesu anatangaza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na dhuluma kwa watu wasiokuwa na hatia. Kwa njia ya imani kwa Kristo Mfufuka, mwanadamu anaweza kupata tena matumaini aliyopokwa kutokana na kukengeuka pamoja na mmong’onyoko wa kimaadili. Ni matumaini ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwamba, mwanga wa Kristo Mfufuka utaweza kuiangazia mioyo ya binadamu, ili kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.