2015-04-10 15:38:00

Ogopa, mkong'oto! Toma, kasepa! Hapa ni kitimtim!


Woga wa kuvamiwa na majambazi au wevi majumbani, ndio unaowafanya watu kujenga nyumba zao kwa kujihami kujengelea milango na madirisha kwa vyuma vigumu (nondo), na nyumba kuwa ngome au gereza. Woga huo unamfanya mwenye nyumba kuwa mfungwa wa nyumba yake mwenyewe. Hofu namna hiyo iliiponza familia moja pale ilipojikuta inateketea kwa moto uliolipuka nyumbani humo, na kushindwa kujiokoa wala kuokolewa toka nje.

Leo tutawashuhudia watu waliojifungia kwa hofu ndani ya chumba kimoja na yaliyowasibu. Tutamwona pia mtu mmoja, asiye na woga na yaliyomsibu. Mambo yalikuwa hivi, kwamba baada ya makashkashi aliyopewa Yesu, ya kushikwa, kuteswa, ya kusulibiwa hadi kufa msalabani. Baada ya mazishi yake wayahudi wakaingia mara moja kwenye sherehe za Pasaka yao (Sabato). Wakati huo wafuasi wale wakaingiwa na woga mkubwa sana, wakajifungia katika chumba kimoja, kama ilivyoandikwa. “Walipokuwapo wanafunzi milango imefungwa kwa hofu ya wayahudi.” Wanafunzi hao wanaye adui mmoja yaani hofu au woga. Walikuwa wanadhani Wayahudi wote walitaka kuwakamata na kuwapatia mkong’oto! Wakajificha!

Mwanafunzi mmoja Tomaso aitwaye Pacha (Didimo) hakuwa katika kundi la wanafunzi waliojifungia humo chumbani. Kwa hiyo kama chumba kingelipuka moto, Tomaso angenusurika. Yaonekana Tomaso hakuona sababu ya kuogopa kitu chochote. Kwa bahati mbaya alipokosekana akaikosa bahati. Yasemwa kuwa jioni ya siku ile ile ya kwanza ya juma, yaani Jumapili ya Pasaka: “Yesu akaja akasimama katikati yao, akawaambia, Amani kwenu.”  Tunaweza kujiuliza maswali kadhaa katika vituko hivi. Mosi, kwa nini Tomaso hakuogopa kama wanafunzi wengine wa Yesu? Ni nani huyo Pacha wa Tomaso katika kumshuhudia Yesu mfufuka?

Ndugu zangu katika Injili ya Yohane, Tomaso anatokea mara tatu. Mara ya kwanza, pale Yesu alipotaka kwenda Yudea alikotafutwa ili kuuawa. Tomaso akawaambia wanafunzi wenzie “twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” (Yoh. 11:16). Hivi mang’amuzi aliyo nayo Tomaso ni ya kufa basi. Nafasi ya pili ni kwenye chumba cha karamu ya mwisho pale Yesu aliposema: “Nami niendako mwaijua njia.” Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?” (Yoh. 14:4). Hapa Tomaso analingana na mtu anayetaka kuelewa mambo. Ama kweli “kuuliza si ujinga.” Angalia jinsi Yesu anavyo jieleza vizuri: “mimi ni njia, na ukweli na uzima.” Nafasi ya tatu ni ya leo.

Kuna sababu mbalimbali zilizowafanya wanafunzi kuwa na woga. Mosi, yaonekana walikuwa na woga wa kifo. Huo ni woga unaotokana na kukata tamaa ya maisha, yaani kutokuwa na mang’amuzi ya ufufuko wa uzima. Mtu anayeelewa ufufuko na uzima, hawezi kuogopa kifo wala wale wanaosababisha mateso na kifo, kwa sababu  wanafunzi hao walishatumwa kama kondoo kati ya chui au mbwa mwitu.

Woga wa pili wa mtu asiye na mang’amuzi ya ufufuo ni kuogopa kupambana na wale wasiompokea Kristu na sera zake za haki na upendo. Hoja nyingine ya kujitenga na kujifungia chumbani ni ya kieolojia. Yaonekana wanafunzi hawa walijisikia kuwa katika mazingira na hali ngeni isiyo ya kawaida mbele ya macho ya watu. Walijiona ni jumuia yenye sera tofauti ya maisha. “Ninyi mwatoka ulimwenguni lakini siyo wa ulimwengu,” yaani waliogopa kutengwa hata pengine kudharauliwa na kudhulumiwa.

Siku hiyo ya kwanza, “Yesu anawaonesha mikono yake na ubavu wake.” Vitu hivyo “mikono na ubavu” siyo vithibiti vya kufufuka kimwili, bali ni vitambulisho tu. Kwa vyovyote wanafunzi wanafurahi kwa vile wameona Kristu kwamba yuko katikati yao. Lakini woga ulibaki palepale, kwani waliendelea kujifungia chumbani. Tomaso hakuwaelewa wenzake kwa nini wajifungie chumbani. Hata hivyo, hakuwa na nia mbaya wala hakuwaelewa vibaya wenzake. Katika mwono huu, Tomaso siyo Pacha wa watu wale wanaodharau jumuia zao, yaani kuna wengine wanajitenga na jumuia na kuiona kama ni jumuia mbovu. Tomaso hakuona sababu kwa nini aogope na kujifungia ndani ya chumba. Kwa hiyo yeye alijitenga na wenzake kwa sababu alisikitika sana moyoni alipokiona kikundi kile cha wanafunzi kuwa kama kimejiaibisha, au kimeleta makwazo na sasa hakiaminiki tena. Walipokuwa na Yesu kikundi kilianza kujulikana na kuheshimika mitaani. Sasa wameanguka.

Kwa hoja hiyo Tomaso ni pacha wa wale wanaojisikia aibu pindi kanisa au dini inapofedheheka kutokana na kupotoka kwa maadili ndani ya kanisa au dini na hivi kukosa kuaminika na kuheshimika. Mapato yake mtu anaona ni afadhali ajitenge kidogo hadi hapo mambo yatakapotengamaa. Tofauti kwa Tomaso ni kwamba alirudi kuangalia hali halisi ya  jumuia yake. Kwa bahati nzuri mara moja alipofika akaambiwa, “Bwana umekosa uhondo, hapa mambo yamebadilika hayapo kama ulivyoyaacha, sisi wenzako tumemwona Bwana.” Hapo Tomaso anaonesha jinsi asivyokuwa mwoga anasema: “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumani, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.” Kisha Yesu anapotokea anamwalika Tomaso “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.”

Hapa tunapambana na Pacha mwingine wa Tomaso, na tunapata mafundisho mawili. Mosi, Pacha wa Tomaso ni yule anayetaka kuhakikisha kwa kuona na kugusa. Yaani Pacha yule anayeona kwa jicho la imani lakini tunataka kusadikishwa na kuhakikishwa. Kwa sisi ambao hatukuishi na Yesu na kumwona kwa macho yetu, tunaalikwa kushuhudia kwa imani yetu ufufuko wa Yesu. Pili, jeraha la ubavu wa Yesu linawakilisha moyo wa upendo, na la mikononi huwakilisha mikono inayochapa kazi ya kutumikia wengine. Hivi Yesu anamwalika kila mwanafunzi kugusa majeraha ya mikononi na ya ubavuni mwake, yaani kupokea mapendekezo yale ya upendo na kusaidia wengine.

Ndugu zangu leo tumetahadharishwa juu ya woga, kwa sababu woga unamkosesha mtu uvumilivu, unakufanya uwe mwonevu, unakugeuza kuwa mtu wa siasa kali ya dini. Mathalani katika kusali au kuhubiri daima mwoga anagumia na kupiga makelele. Mtu mwoga hataki majadiliano yaliyotulia. Mtu mwoga hana uhakika wa wa mambo. Mwoga anajifungia katika mwenyewe na kujihami kwa mficho. Huko ndiko kujilipua mwenyewe ndani ya gereza ulilojitengenezea. Kumbe mtu asiye mwoga huyo anao uhakika na anaufahamu ukweli na anauishi waziwazi na hawezi kugumia bali anahubiri kwa utulivu. Utulivu huo ndiyo mbinu nzuri inayoweza kuwasaidia wengine kuangalia  ukweli wa mwanga wa Pasaka.

Woga unatufanya tujifungie ndani ya chumba na kujidanganya katika mambo ambayo hayana msingi wa ukweli.  Woga unatuogopesha dhidi ya kila kosoo itokayo nje ya jumuia zetu. Tunakuwa na hofu ya kuingiliwa na watu wa imani kali, watu wa siasa kali, wataalamu wanaokosoa dini yetu nk. Mathalani woga ule uliowawahi kuwaingia wakatoliki pale biblia ilipochukuliwa na waprotestanti, au woga dhidi ya demokrasia, au woga wa kuingiliwa na utamaduni mgeni, au wa mambo mapya yanayotutaka kufanya marekebisho katika dini. Woga aina hiyo ndio uliowakumba wanafunzi wa Yesu hadi wakajifungia ndani ya chumba huku wakidhani kwamba watu wote ni adui.

Pacha wa Tomaso daima atajidhihirisha katika jibu la imani kuu analolitoa Tomaso: “Bwana wangu na Mungu wangu!” yaani kuungama imani. Tomaso ameona vithibiti vya upendo, kwamba amemwona Mungu kweli aliyesulibiwa kwa ajili ya upendo ubavuni na mikononi. Hayo ndiyo mapato ya kuangalia majeraha ya Yesu kwa jicho la imani. Hutakuwa tena na woga wowote wa kupenda na kutumikia kwa jina la Kristu. Sisi tunamgusa Yesu katika mkate na divai vilivyogeuzwa kuwa mwili na damu yake kwa ajili ya kutupenda. Tumshuhudie kwa moyo na kwa matendo yetu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.