2015-04-10 12:34:00

Jimbo Katoliki Shinyanga, mmepata Jembe la nguvu, shikamaneni naye!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni kati ya viongozi wa Kanisa wanaotarajiwa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumweka wakfu na hatimaye, kumsimika Askofu mteule Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Jumapili ya huruma ya Mungu hapo tarehe 12 Aprili 2015, Jimboni Shinyanga.

Askofu mkuu Rugambwa, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, anapenda kumshukuru Mungu kwa zawadi kubwa ya Askofu mteule Sangu ambaye amefanya kazi katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwa muda wa miaka minane. Viongozi wa Kanisa wameridhika sana na utumishi wake mwanana, wenye ubora na viwango. Ni Askofu mteule Sangu amefundwa akafundika sasa anakabidhiwa kazi ya kufundisha, kuongoza na kuwatakasa watu wa Mungu Jimbo Katoliki Shinyanga.

Askofu mkuu Rugambwa anakiri kwamba, Uaskofu ni kazi na utume mgumu unaohitaji kwa namna ya pekee ushirikiano na mshikamano wa dhati na Familia ya Mungu. Kumbe, anachukua fursa hii kuitaka Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Shinyanga, kumpokea na kumwonesha ushirikiano wa dhati Askofu mteule Liberatus Sangu wakati atakapoanza kutekeleza dhamana na utume wake kama Askofu wa Shinyanga. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kazi ya Mungu Jimbo la Shinyanga na Tanzania katika ujumla wake inasonga mbele kwa ufanisi mkubwa.

Kardinali Fernando Filoni pamoja na viongozi wakuu waandamizi na wafanyakazi wote wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wanamtakia kheri na baraka Askofu mteule Liberatus Sangu katika maisha na utume wake miongoni mwa Familia ya Mungu Jimboni Shinyanga.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.