2015-04-09 15:22:00

Watawa wakiwezeshwa kwenye elimu watacharuka katika maendeleo endelevu


Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi za Roho Mtakatifu katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha baadhi ya changamoto ambazo Mashirika ya Kitawa yanakumbana nayo Barani Afrika. Mashirika mengi yanafanya kazi za kujitolea katika kuhudumia Familia ya Mungu kwenye Majimbo na Parokia mbali mbali, changamoto hapa ni kwa Maaskofu na Mapadre kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuwategemeza watawa wanaofanya kazi katika Majimbo na Parokia zao pale inapowezekana, hata ikishindikana, bado watawa wataendelea kutekeleza dhamana na utume wao ndani ya Makanisa mahalia.

Sr. Maria Eugenia Thomas anasema, watawa wengi wanategemea sana shughuli za kilimo na ufugaji kwa ajili ya kujitegemea. Lakini kutokana na changamoto mbali mbali katika sekta ya kilimo, bado watawa wanasua sua sana katika masuala ya kilimo na ufugaji. Jambo la msingi kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanawekeza katika majiundo makini na endelevu kwa watawa pamoja na kuhakikisha kwamba, wanapatiwa elimu ya juu katika medani mbali mbali ili kusaidia maboresho na mikakati ya kujitegemea.

Watawa wakiwezeshwa kielimu wataweza kusimamia na kuendeleza miradi mbali mbali inayoanzishwa na mashirika yao na hivyo kupunguza gharama ya uendeshaji. Kwa njia hii watawa wanaweza kuendelea pia kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sadaka na majitoleo yao, vinginevyo itakuwa ni vigumu sana kwa siku za usoni kutokana na ushindani uliopo kwa sasa.

Elimu makini isaidie kuwakomboa watawa na kuwajengea uwezo wa kupambana na mazingira, ili kweli maisha yao yawe na mvuto na mashiko kwa vijana wa kizazi kipya. Watawa wakijikwamua kiuchumi, wataweza kuwaendeleza jirani zao, maskini na wote wanaohitaji msaada wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.