2015-04-09 10:38:00

Tafakarini yaliyopita kwa shukrani, kumbatieni ya sasa kwa hamasa!


Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza watawa katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani; kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Haya ndiyo mambo msingi ambayo yamesemwa na Kardinali Joao Braz de Avis, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume wakati wa kufungua kongamano la malezi kimataifa, Jumatano, 8 Aprili 2015 kwa kutambua kwamba, Kanisa zima liko pamoja nao katika kipindi hiki.

Malezi ni mchakato unaogusa undani wa mwanadamu, mahusiano yake na Mwenyezi Mungu pamoja na ndugu zake katika Kristo. Changamoto iliyoko mbele ya watawa ni kuhakikisha kwamba, wanaendeleza hija ya maisha iliyoanzishwa na Mitume pamoja na waasisi wa Mashirika yao ya Kitawa na Kazi za Kitume; kwa kuangalia changamoto, magumu na vizingiti vilivyoko kwa wakati huu; daima wakidumisha matumaini na uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Watawa wanahamasishwa kuendelea kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuwa na matumaini makubwa kwa kazi ya Roho Mtakatifu na kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani. Watawa katika historia ya maisha yao, wamejitahidi kusoma alama za nyakati na kumwilisha karama katika maisha na utume wa Kanisa. Leo hii wanakabiliwa na mazingira, tamaduni na utambulisho mpya; mambo yanayohitaji wongofu wa ndani pamoja na kuendelea kujikita katika malezi makini ya awali na endelevu kama walivyokazia Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kardinali De Avis anasema kwamba, kuna haja kwa watawa kuendeleza hija ya upyaisho wa maisha kadiri ya mwanga wa Roho Mtakatifu. Watawa wanapaswa kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa unyenyekevu na upendo mkuu; kwa kushuhudia kwa furaha utakatifu wa maisha. Huu ni mwaliko pia kwa watawa kuyaishi ya sasa kwa hamasa kuu, kwa kujikita na kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha, ili kupenda kama Kristo alivyopenda; kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji na utamadunisho kama walivyofanya waasisi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume; katika umoja, udugu na mshikamano kadiri ya mpango wa Mungu.

Kardinali De Avis anasema kwamba, ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinajikita katika “Falsafa ya mwenye nguvu mpishe” ukosefu wa usawa na haki; uvunjwaji wa haki msingi na utu wa binadamu. Hapa Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kutafuta njia na mbinu muafaka za kuweza kuishi kwa umoja, udugu na mshikamano; daima wakiyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito; ongezeko kubwa la watawa wenye umri mkubwa, ukata, changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; mawazo mepesi mepesi; ubaguzi na magumu ya maisha. Hapa ni mahali pa kuwekeza matumaini bila ya kukata tamaa, kwani Yesu mwenyewe amewahakikishia wafuasi wake kwamba, atakuwa pamoja nao hadi utimilifu wa dahali. Haya ni matumaini yasiyodanganya kamwe na watawa wanaweza kuendelea kuandika historia ya maisha na utume wao hata kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.