2015-04-09 14:54:00

Jimbo Katoliki Shinyanga, vumbi limeanza kutimuka! Tunakuja kuwashika!


Askofu mteule Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa rasmi kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Shinyanga, katiba Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika Jimboni Shinyanga, katika Kanisa la Bikira Maria, Mama wa huruma, Ngokolo, Shinyanga.

Katika hotuba yake ya kuagana na Jumuiya ya Wanafunzi Watanzania Wakatoliki wanaosoma na kutekeleza utume wao mjini Roma aliwashirikisha jinsi ambayo katika maisha yake ameguswa kwa karibu zaidi na upendo wa Mungu, tangu alipokuwa Seminarini, alipokuwa anajiandaa kwa Daraja la Ushemasi hadi pale alipopewa Daraja Takatifu. Anafafanua alama mbali mbali zilizoko kwenye Nembo yake ya Uaskofu inayoongozwa na kauli mbiu “ Tunda la Roho ni upendo” ambao ni muhtasari wa yote.

Anabaianisha karama na sifa za upendo wa Kimungu katika maisha ya mwanadamu na kwa namna ya pekee anasimulia jinsi ambavyo kwa njia ya Marehemu Askofu Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga alivyoguswa na upendo wa Mungu ambao umemgeuza na kumfanya jinsi alivyo leo hii. Huu ndio upendo anaotaka kuishirikisha Familia ya Mungu Jimboni Shinyanga. Jimbo Katoliki Sumbawanga, ameliachia zawadi ya kujikita katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Askofu mteule Sangu anabainisha  kwamba, mahali penye upendo wa kweli hapo kuna amani, mshikamano na haki. Ndiyo maana anataka kuwahamasisha wananchi wa Shinyanga kujikita katika Injili ya uhai kwa kutetea na kuthamini zawadi ya maisha; kwa kuwajali walemavu wa ngozi na pamoja na wazee ambao kwa miaka kadhaa wamekuwa ni wahanga wa imani za kishirikina. Watu wapendane kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, wanachangamotishwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.