2015-04-08 09:31:00

Malezi yajikite katika Neno la Mungu: mwaalimu, mwanga na furaha!


Kongamano la walezi wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, limefunguliwa rasmi, Jumanne jioni tarehe 7 Aprili kwa mkesha wa sala ambao umehudhuriwa na walezi 1200 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ni walezi wanaotoka katika mataifa, lugha na tamaduni mbali mbali ambao kwa pamoja wanapenda kuchambua kwa kina na mapana changamoto za malezi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ibada ya mkesha imeongozwa na Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya kitawa na kazi za kitume. Mkesha huu umegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza imekua ni maandamano ya watawa wakiwa wamebeba Mshumaa wa Pasaka, changamoto na mwaliko kwa watawa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili awaangazie katika utekelezaji wa dhamana nyeti ya malezi kwa watawa katika mashirika yao.

Sehemu ya pili, imejikita katika kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu ambalo linapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini. Neno la Mungu limetangazwa kwa lugha mbali mbali za kimataifa pamoja na kuonesha kwamba, Neno la Mungu linapaswa kuwa ni kiini cha majiundo makini ya watawa ndani ya Kanisa.

Sehemu ya tatu, imesimikwa katika kulitafakari Neno la Mungu linalowafunda watawa katika maisha na utume wao. Walezi wanapaswa kukumbuka kwamba, wao ni madaraja kati ya uhuru wa binadamu na uhuru wa Mungu. Malezi na majiundo ya kitawa hayana budi kugusa: akili, mioyo na mikono na hatimaye, kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Lengo ni kuwawezesha watawa kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo kwa kukumbatia Injili inayogeukwa kuwa ni chachu ya maisha.

Mkesha huu ulikuwa ni fursa pia kwa watawa kutoka mashirika mbali mbali kubadilishana uzoefu na mang’amuzi katika mchakato wa malezi ya kitawa na kazi za kitume. Kwa pamoja wamekazia umuhimu wa malezi ya awali na malezi maalum kwa kila shirika ili kupambana na changamoto za maisha katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.