2015-04-08 15:39:00

Kardinali Turcotte, kiongozi mahiri na shupavu amefariki dunia


Baba Mtakatifu Francisko amepokea taarifa za kifo cha Kardinali Jean Claude Turcotte, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Montreal kwa masikitiko na majonzi makuu kwani anamkumbuka jinsi alivyokuwa mchungaji mahiri, aliyejisadaka bila ya kujibakiza, akajifunga kibwebwe kupambana na changamoto za maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo kwa ujasiri, moyo na ari kuu. 

Kardinali Turcotte amefariki dunia tarehe 8 Aprili 2015 akiwa na umri wa miaka 78. Alichapa kazi sana wakati alipokuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, alichangia sana katika maadhimisho ya Sinodi ya Maisha ya kuwekwa wakfu iliyoadhimishwa kunako mwaka 1994 na Sinodi maalum kwa ajili ya Kanisa Barani Amerika, iliyoadhimishwa kunako mwaka 1997. Alishiriki kama Rais kwa ajili ya kuandika ujumbe kwa Familia ya Mungu.

Marehemu kardinali Turcotte alizaliwa kunako tarehe 26 Juni 1936. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikuhani, akapewa Daraja Takatifu la Upadre kunako mwaka 1959. Alikuwa ni Padre mchapakazi aliyependa kujiendeleza katika masuala ya shughuli na mikakati ya kichungaji. Kunako mwaka 1981 aliteuliwa kuwa ni Makamu Askofu, Jimbo kuu la Montreal. Mwezi Aprili 1982 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Montreal na kuwekwa wakfu kama Askofu kunako tarehe 29 Juni 1982.

Kunako mwaka 1990 Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Montreal. Mtakatifu Yohane Paulo kunako tarehe 26 Novemba 1994 akamteuwa kuwa Kardinali. Kutokana na kifo cha Kardinali Turcotte, kwa sasa Dekania ya Makardinali imebaki na Makardinali 225 kati yao 122 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na wengine 103 hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura kutokana na umri wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.