2015-04-08 11:19:00

Acheni imani za kishirikina, kumbatieni Injili ya uhai na haki msingi!


Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania anabainisha kwamba, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Afrika Mashariki yanatokana na imani za kishirikina ambazo zinapelekea baadhi ya watu ndani ya jamii kuamini kwamba, kwa kutumia viungo vya walemavu wa ngozi wanaweza kupata utajiri wa haraka haraka, kinga na madaraka; mambo ambayo hayana ukweli wowote.Imani za kishirikina zimekuwa ni chanzo cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Hapa kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kukumbatia zawadi ya maisha, utu na heshima ya binadamu pamoja na kukazia haki msingi za binadamu. Mauaji ya walemavu wa ngozi ni kukumbatia utamaduni wa kifo.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya ameishauri Serikali ya Tanzania kutumia fursa ya kuahirishwa kwa zoezi la kura ya maoni kwa ajili ya Katiba inayopendekezwa kama ilivyoamriwa na Tume ya uchaguzi nchini Tanzania, ili kuwaelimisha wananchi mambo msingi yaliyomo kwenye Katiba inayopendekezwa, ili waweze kupiga kura kwa busara zaidi. Serikali iwe na ujasiri wa kubainisha kasoro na mapungufu yaliyojitokeza katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba inayopendekezwa, ili kuzirekebisha kasoro hizi, hatimaye, watanzania waweze kupata Katiba makini ambayo itakuwa ni kiungo muhimu na sheria mama kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Iwe ni Katiba inayotokana na wananchi wenyewe kwa ajili ya ustawi wao.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya anawaalika watanzania wenye sifa za kujiandikisha kupiga kura kutekeleza dhamana na wajibu wao kisheria, ili waweze kujitokeza kushiriki katika zoezi la kupiga kura wakati utakapowadia. Lengo ni kuwapata viongozi wema, waadilifu, wakweli na wanaotoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya watanzania wengi. Tanzania ikiwapata viongozi bora na wachapakazi, wataweza kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watanzania wengi katika medani mbali mbali.

Na Rodrick Minja,

Dodoma.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.