2015-04-07 11:47:00

Wanawake ni waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi


Wanawake sehemu mbali mbali duniani ni wadau wakuu katika kulinda na kutunza mazingira, kwani hawa ndio watu wanaotambua madhara ya uharibu wa mazingira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni watu wanaoguswa kwa karibu sana na mahangaiko ya watoto wenye utapiamlo wa kutisha, baa la njaa, umaskini pamoja na magonjwa. Kumbe si kweli kwamba, masuala ya utunzaji bora wa mazingira ni dhamana ambayo inatekelezwa na wanasiasa au vikundi vya watunza mazingira, lakini ikumbukwe kwamba, hata wanawake wamo hata kama hawasikiki sana.

Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujadili kuhusu matatizo, fursa na changamaoto zinazoendelea kujitokeza duniani: Nishati ya atomiki na madhara yake katika ustawi na maendeleo ya binadamu; ongezeko la hewa ya ukaa inayotishia usalama na maisha ya watu wengi duniani; ni mambo yanayomgusa mwanamke katika undani wa maisha yake: kiroho na kimwili. Ndiyo maana kuna uhusiano mkubwa kati ya mazingira, wanawake na Kanisa.

Mama Kanisa anapohimiza utunzaji bora wa mazingira anapania kwa namna ya pekee kuwalinda na kuwatetea wanyonge na maskini kwani hawa ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi. Madhara ya uchafuzi wa vyanzo vya maji yanawagusa kwa namna ya pekee wanawake na watoto, kwani  mahangaiko yote ya kifamilia atayabeba mwanamke kwa imani na matumaini.

Ni wanawake ambao wanaathirika vibaya pale ambapo hakuna sera nzuri za umilikaji wa ardhi kwani wao ndio wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula na biashara kwa familia zao. Pale maeneo makubwa ya ardhi yanapokwapuliwa kwa ajili ya kilimo cha nishati uoto kwa ajili ya kujipatia  faida kubwa, wanawake wanateseka sana. Ni matumaini ya waamini kwamba, Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko utaweza kuweka bayana mahusiano yaliyopo kati ya maisha ya kiroho na utunzaji bora wa mazingira kwani Mwenyezi Mungu alimkabidhi binadamu dhamana ya kutunza na kuendeleza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote.

Bila shaka Baba Mtakatifu ataendelea kuonesha madhara makubwa ya uchafuzi wa mazingira katika maisha ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezon mwa jamii. Kumbe, utunzaji bora wa mazingira hauna budi kuwa ni sehemu ya mchakato wa maisha ya kiroho na wala si suala la kisiasa na kitamaduni. Waamini wanachangamotishwa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira, sanjari na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Itakumbukwa kwamba, maskini na watu wengi wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni wanawake na watoto!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.