2015-04-06 11:42:00

Mapadre na Watawa: Wahudumieni Watu wa Mungu pasi na kujibakiza!


Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuwahudumia Watu wa Mungu kwa kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakasa kwa kutambua kwamba, wao wamepewa dhamana ya kuhudumia Neno la Mungu na kuadhimisha Sakramenti za Kanisa.  Huduma hii ya Kikuhani kwa Familia ya Mungu haina budi kutolewa bila kugubikwa na ubinafsi, uchoyo wala masilahi binafsi, kwani Makuhani wamepakwa mafuta kwa ajili ya huduma kwa Familia ya Mungu.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Kardinali Mario Aurelio, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires wakati wa Maadhimisho ya Alhamisi kuu, Kanisa lilipokuwa linakumbuka siku ile iliyotanguliwa kuteswa kwake, Yesu Kristo alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na huduma ya upendo kwa jirani. Ari na mwamko wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa haina budi kuonekana kila wakati Makuhani wanapoadhimisha Sakramenti za Kanisa, kwa imani, matumaini na furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Makuhani watambue kwamba, wamepakwa mafuta ili kumtumikia Kristo na Kanisa lake bila ya kujibakiza hata kidogo.

Waamini nao kwa upande wao, wanapaswa kujivunia hali ya kuwa ni Wakristo, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mguso na kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wamepewa bure, nao wanapaswa kuwashirikisha jirani zao kwa njia ya ukarimu unaomwilishwa katika ushuhuda wa maisha. Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki katika: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo, kumbe wanatumwa kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha na Matumaini.

Kardinali Mario Aurelio amegusia kwa kina na mapana dhamana na utume wa watawa katika Kanisa. Watawa ni watu ambao katika historia ya maisha na utume wa Kanisa wamekubali na kukumbatia upendo wa Kristo ambao wamediriki kuwashirikisha watu wengine sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Ni huduma ambayo inaendelea kujionesha katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya binadamu. Watawa wamekuwa ni faraja na matumaini kwa maskini, yatima na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, watu wengi wamegundua kwamba, wao ni mawe hai yanayopaswa kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Watawa ni kundi ambalo limeendelea kulisindikiza Kanisa kwa njia ya sala na sadaka katika mchakato wa utekelezaji wa dhamana ya kimissionari walioachiwa na Kristo Mfufuka. Watawa ni kielelezo cha huduma ya Kanisa kwa walimwengu, hasa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watawa ni kielelezo makini cha Msamaria mwema, anayejisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo, imani na matumaini. Ni watu wanaotumia rasilimali muda kwa ajili ya kuwasikiliza na kuwafariji Watu wa Mungu, hata pengine kwa uwepo wao wa karibu tu! Watawa ni alama ya baraka na neema ya Mungu kwa waja wake, kumbe wanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kusaidiwa katika maisha na utume wao, ili waendelee kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.