2015-04-06 10:54:00

Kardinali Filoni: Cheche za matumaini wakati wa Maadhimisho ya Pasaka!


Nchi ya Iraq ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa fujo, vurugu na mauaji ya kikatili wakati wa mkesha na hatimaye maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, waamini wamefurika kwenye Makanisa mbali mbali nchini humo. Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko huko Iraq kama kielelezo cha mshikamano wa udugu na upendo wa dhati.

Kardinali Filoni ameadhimisha Siku kuu ya Pasaka kwa maelfu ya Wakristo kwenye Kambi ya wakimbizi ya Erbill na kuhudhuriwa pia na Askofu mkuu Giorgio Lingua, Balozi wa Vatican nchini Iraq. Maadhimisho haya ni kielelezo cha imani na matumaini kwa Wakristo huko Iraq wanaoendelea kuteseka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hawana sababu ya kukata tamaa licha ya kuendelea kuishi na kuhudumiwa wakati huu katika kambi za wakimbizi. Kwa sasa viongozi mahalia wanafanya jitihada za kuwahamishia wakimbizi hawa katika makazi mapya, ili kulinda na kuendeleza utu na heshima yao. Kardinali Filoni anasema inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wanazidi kushambuliwa na magonjwa ya milipuko.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa ujumbe wake kwa mji wa Roma na Dunia kwa ujumla, “Urbi et Orbi” kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewakumbuka kwa namna ya pekee Wakristo huko Iraq, Syria na Nigeria na Kenya na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasitisha biashara ya silaha huko Mashariki ya Kati ambayo kwa sasa imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa ya watu wasiokuwa na hatia. Ameishauri Jumuiya ya Kimataifa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kuteseka nchini Iraq na sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.