2015-04-06 10:20:00

Breaking News: Yesu amefufuka kweli kweli Alleluiya!


Asubuhi na mapema siku ya kwanza ya juma, wanawake walikwenda karibuni kuangalia mahali alipozikwa Yesu, wakapigwa na mshangao kuona Kaburini liko wazi na Malaika akawaambia kwamba, Yesu amefufuka kutoka katika wafu na kwamba, walipaswa kwenda kuwajulisha ndugu zake kwamba amefufuka katika wafu. Tazama amewatangulia kwenda Galilaya, ndiko watakakomwona. Galilaya  ni mji uliokuwa pembezoni, mahali ambapo Yesu alianza kutekeleza utume wake na hapa ni mahali pa kwanza pa kutangazia Injili ya Ufufuko wa Kristo, ili watu wote waweze kukutana na kuonana na Yesu Kristo Mfufuka anayeendelea kutenda katika historia.

Tafakari hii imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu ya Oktava ya Pasaka, tarehe 6 Aprili 2015 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu. Baba Mtakatifu anasema kwamba, Kanisa linaendelea kutangaza kwamba, Yesu amefufuka na kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wameifia dhambi na kufufuka katika maisha mapya; kutoka katika utumwa wa dhambi na kuwa huru katika upendo, Habari Njema ambayo waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuipeleka kwa Watu wa Mataifa. Ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya matumaini na kwamba, Kanisa litaendelea kutangaza Fumbo la Pasaka si tu kwa maneno bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha hususan kwa wale wanaotafuta furaha ya kweli.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Oktava ya Pasaka ni siku ambazo Wakristo wanahamasishwa kuingia na kulitafakari Fumbo la Pasaka, ili neema na baraka za Kristo Mfufuka ziweze kuacha chapa katika mioyo na maisha ya waamini. Pasaka ni tukio ambalo limeleta mageuzi makubwa kwa binadamu na historia ya dunia. Huu ni ushindi wa maisha dhidi ya kifo; ni mwanzo wa maisha mapya. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajiachilia mbele ya Kristo, ili nguvu ya Pasaka iweze kuwaletea mabadiliko.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Sala ya Malkia wa Mbingu ni chemchemi ya wimbo wa Alleluiya, changamoto ya kuungana na Bikira Maria kufurahia ufufuko wa Mwanaye mpendwa, yule ambaye alimbeba tumboni mwake, amefufuka kweli kweli kama alivyosema. Furaha ya Bikira Maria ni chemchemi ya furaha kwa waamini, kwani ni Mama ambaye alitunza moyoni mwake imani na matukio makuu ya maisha na utume wa Yesu.

Mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Baba Mtakatifu alitambua uwepo wa Kikundi cha Shalom ambacho kinafanya kampeni ya hadhara kuhusu mateso na nyanyaso za Wakristo huko Mashariki ya Kati, hii haina budi kuwa ni hija ya maisha ya kiroho inayojikita katika sala sanjari na kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea Wakristo huko Mashariki ya Kati. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haitaendelea kukaa kimya na kuangalia mauaji, mateso na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Furaha ya Ufufuko wa Kristo iwe ni sababu kwa waamini kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Baba Mtakatifu amewatakia wote Pasaka Njema na kuwaomba kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.