2015-04-05 10:35:00

Uganda: mauaji, vipigo na nyanyaso dhidi ya wanawake vinachafua Pasaka


Familia nyingi  nchini Uganda badala ya kuserebuka na kumshangilia Kristo mfufuka, zinajikuta zinakuwa ni uwanja wa mapambano na nyanyaso mbali mbali; familia badala ya kuwa ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu, zimegeuka kuwa ni chanzo cha vilio na simanzi kuu inayojikita katika maisha ya wanafamilia wengi. Ni masikitiko makubwa yanayotolewa na Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala Uganda, katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Pasaka kwa mwaka 2015.

Dhuluma na nyanyaso ni laana kubwa katika familia nyingi nchini Uganda, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanabadili mwelekeo wa maisha kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kuanzia ndani ya familia husika. Wananchi watambue kwamba, familia inapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu. Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka, iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha tunu bora za maisha ya ndoa na familia, kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, ili kweli Familia za Kikristo ziweze kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Askofu mkuu Lwanga anasema, Uganda inaendelea kukabiliwa na matatizo lukuki dhidi ya haki msingi za binadamu pamoja na utu wema. Kuna mauaji ya kinyama yanayoendelea kutendeka siku kwa siku; kuna biashara haramu ya binadamu inayoendelea kupamba moto, jambo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, kuna mauaji ya watoto wadogo kwa kisingizio cha imani za kishirikina bila kusahau saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma.

Familia badala ya kuwa ni mahali pa faraja na kitulizo, zimegeuka kuwa ni mahali pa kuchumia majanga badala ya amani na upendo. Ukatili wa majumbani anasema Askofu mkuu Lwanga ni jambo linaloharibu maisha ya kifamilia, kikanisa na kijamii. Familia inapaswa kuwa ni shule ya upendo, haki na amani; mahali ambapo watu wanajifunza kupenda na kupendwa; kusamehe na kusamehewa, lakini mambo ni kinyume kwa familia nyingi nchini Uganda.

Familia iwe ni mahali ambapo watu wanapendana na kuhusiana vyema na jirani zao. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kubadili tabia na maisha kwa kujikita katika utu wema, upole na unyenyekevu. Ni changamoto ya kuachana na tabia, mila na desturi zilizopitwa na wakati kwa kudhani kwamba, kipigo kwa wanawake ni dalili za upendo wa dhati! Vipigo na nyanyaso ndani ya familia nyingi zimesababisha watu kupoteza maisha na wengine kupata vilema vya kudumu.

Vitendo vya kigaidi bado vinaendelea kuwa ni tishio kwa usalama wa maisha ya watu wengi Afrika Mashariki, kama ilivyotokea kwenye Chuo Kikuu cha Garissa, nchini Kenya, wanafunzi 147 wamepoteza maisha na kwamba, kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao hadi sasa hawajulikani mahali walipo. Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linaendelea kusubiri kwa imani na matumaini kuhusu taarifa rasmi za hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.